Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jinsi shughuli za kibinadamu zinavyotishia uhai wa Ziwa Victoria

11585 Pic+uhai TanzaniaWeb

Mon, 13 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bonde la Ziwa Victoria lenye ukubwa wa kilomita za mraba 68, 800 ndilo bonde kubwa kuliko yote barani Afrika na linashika nafasi ya pili duniani nyuma ya Bonde la Superior la Amerika Kaskazini.

Bonde hili ni kati ya maeneo muhimu na ya kimkakati kiuchumi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupitia sekta za uvuvi, usafirishaji, utalii na kilimo cha umwagiliaji.

Shughuli hizo zinafanyika ndani na kwenye mwambao wa Ziwa Victoria lililo futi 3, 726 kutoka usawa wa bahari.

Zaidi ya watu 35 milioni wanaoishi ukanda wa bonde la Ziwa Victoria katika mataifa ya Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan, Ethiopia na Misri wanaaminika kujihusisha na shughuli za uvuvi ndani ya ziwa hilo ambalo ni chanzo cha Mto Nile unaomwaga maji yake ndani ya Bahari ya Mediterranean, umbali wa zaidi ya maili 4, 000.

Kwa mujibu wa mgawo wa Kimataifa, Tanzania inamiliki sehemu kubwa ya Ziwa Victoria ikiwa na asilimia 51 ikifuatiwa na Uganda inayomiliki asilimia 43 huku Kenya ikiwa na asilimia sita ya ziwa lote.

Utajiri na rasilimali inayopatikana ndani ya Ziwa Victoria ni miti mingi iliyo ndani ya bonde lake na samaki na maji baridi.

Mikoa iliyoko ndani ya bonde la Ziwa Victoria kwa upande wa Tanzania ni Mwanza, Mara, Simiyu, Shinyanga, Geita na Kagera.

Mito mikubwa ya Kagera, Simiyu, Mbarageti, Gurmeti, Rubana, Mara na mto Mori inamwaga maji yake ndani ya Ziwa Victoria na hivyo kuwa miongoni mwa sehemu ya uhai wa ziwa hilo.

Hata hivyo, uwingi wa shughuli za kibinadamu ndani ya ziwa lenyewe na katika bonde lake zinatishia si tu uhifadhi wa mazingira, bali pia upatikanaji na kiwango cha maji ndani ya ziwa na chini ya ardhi katika eneo lote la bonde la Ziwa Victoria.

Athari ya shughuli za kibinadamu

Uchimbaji holela wa visima vifupi na virefu vya maji pamoja na mabwawa ni miongoni mwa shughuli za kibinadamu zinazotishia uhai wa bonde na ziwa lenyewe.

Kwa mujibu wa Tovuti Kuu ya taarifa za Serikali (www.opendata.go.tz), hadi Novemba 2016 kulikuwa na zaidi ya visima 100 mikoa ya Mwanza, Mara na Kagera pekee.

Mwanza ukiwa kinara kwa kuwa na visima 81 ikifuatiwa na Mara visima 15 na Kagera ikiwa na vinne.

Kwa upande wa mabwawa, mkoa wa Mara unashika nafasi ya kwanza kwa kuchimba mabwawa 51, ikifuatiwa na Mwanza 47, Shinyanga 32 na Kagera tisa na hivyo kufanya jumla ya mabwawa katika mikoa hii minne kufikia 139.

Ukataji miti hovyo, kuchoma mkaa, ufugaji na kilimo kisichozingatia uhifadhi endelevu wa mazingira ni kati ya shughuli nyingine za kibinadamu zinazoharibu kingo na vyanzo vya mito inayomwaga maji yake ndani ya Ziwa Victoria.

Uharibifu wa chanzo na kingo za mto Mara katika maeneo ya wilaya ya Serengeti ni baadhi changamoto zinazoonekana dhahiri katika ukanda wa bonde la ziwa hilo.

Tayari uongozi wa Serikali wilaya ya Serengeti kwa kushirikiana na wadau wengine umeanzisha na kutekeleza kampeni ya kupanda zaidi ya miti 10,000 kwenye kingo za mto Mara.

Katibu tawala wilaya ya Serengeti, Cosmas Qamara anasema mpango huo ambao tayari umefanikisha kupandwa miti zaidi ya 8, 000 unahusisha pia utungaji wa sheria ndogo kuwadhibiti wasiozingatia ufugaji, uvuvi na kilimo endelevu unaotunza na kuhifadhi mazingira ya mto huo unaoanzia katika hifadhi ya Maasai Mara nchini Kenya.

Mto huo ni kati ya mito inayotiririsha maji yake ndani ya Ziwa Victoria ikipitia wilaya za Serengeti, Tarime, Rorya na Butiama, zote za mkoani Mara.

Mkurugenzi wa Asasi ya Tumaini Jema inayoashirikiana na Serikali katika kampeni hiyo, Shukurani Rwambali anasema pamoja na wananchi wa kawaida, mpango wa kupanda miti pia unawalenga wanafunzi katika shule za msingi na sekondari wilayani Serengeti.

“Tunataka kuwalea, kuwakuza na kuwajengea watoto wetu utamaduni wa kupanda miti, kutunza na kuhifadhi mazingira kuanzia shuleni na majumbani. Tumeshapanda zaidi ya miti 8,000 katika maeneo ya shule na kijiji cha Marasomoche inayopakana na mto Mara,” amesema Rwambali

Ofisa misitu wilaya ya Serengeti, Aloyce Paschal anataja mbinu nyingine inayotumika kuhamasisha utunzaji na uhifadhi mazingira kuwa ni elimu kwa umma kupitia mikutano ya hadhara, warsha, semina na kongamano.

“Nia ni kuwa na umma utakaohifadhi na kulinda bonde la Ziwa Victoria kwa matumizi endelevu ya kijamii na kiuchumi,” anasema Paschal.

Sh3 bilioni kutafiti kiasi cha maji bonde la Ziwa Victoria

Baada ya kubaini ongezeko la matumizi ya maji na shughuli za kibinadamu ndani na nje ya ziwa, Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria imepanga kutumia zaidi ya Sh3 bilioni kufanya utafiti wa kiwango cha maji katika mikoa yote ya Kanda ya Ziwa inayounda bonde hilo.

Pamoja na mambo mengine, utafiti huo unalenga kudhibiti matumizi holela na majanga yanayoweza kulikabili Taifa iwapo maji yataendelea kupungua ndani ya bonde hilo upande wa Tanzania.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalum ofisini kwake hivi karibuni,

Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Florence Mahay anasema tayari bajeti ya kazi hiyo ya utafiti ambayo hata hivyo hakutaja kiasi cha fedha kilichotengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19.

“Utafiti kujua kiasi cha maji kwenye mabonde ya maji nchini hufanyika kila baada ya miaka mitano kutegemeana na bajeti ya Serikali ili kujua kiasi cha maji kilichopo, muda wake wa matumizi, kuyapangia matumizi endelevu na kuhadharisha umma kuhusu matumizi holela,” anasema Mahay

Anasema tafiti hizo zinazohusu kina na kiwango cha maji ndizo huziongoza bodi za maji wakati wa kupanga, kugawa na kuidhinisha matumizi ya maji.

Mkurugenzi huyo anasema utafiti kama huo tayari umefanyika katika bonde la Ziwa Rukwa na kubaini hatari ya eneo hilo kukabiliwa na upungufu wa maji ifikapo mwaka 2035 iwapo matumizi holela na uharibifu wa mazingira hayatadhibitiwa ipasavyo.

Mabonde ya mito ya Rufiji na Ruvu kwa mujibu wa Mahay ni maeneo mengine nchini yanayokabiliwa na upungufu wa maji kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji yanayochukua sehemu kubwa ya maji kulinganisha na shughuli nyingine.

“Bonde la Ziwa Tanganyika ndilo bado lina maji mengi kutokana na kuwa na matumizi madogo kulinganisha na mabonde mengine nchini,” anasema Mahay

Mtaalam huyo wa masuala ya maji naishauri Serikali na mamlaka nyingine kuhakikisha kunakuwepo uwiano kati ya matumizi ya maji kwa shughuli za binadamu na kiuchumi kama kilimo cha umwagiliaji na kufua umeme ili kupunguza changamoto ya uhaba wa maji unaoweza kulikabili Taifa siku zijazo.

Wanaochimba visima bila vibali

Kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa maji namba 11 ya mwaka 2009, mtu yeyote anayetiwa hatiani kwa kosa la kuharibu chanzo cha maji, kuchimba kisima bila kibali kutoka bodi ya bonde la maji na anayeficha au kutoa taarifa za uongo kuhusu uharibifu wa chanzo au miti anastahili faini ya Sh500, 000.

“Sheria hiyo pia inatoa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela au vyote viwili, faini na kifungo,” anasema Mahay.

Waonja adha ya maji kupungua

Mwanza ni kati ya mikoa inayopatikana ndani ya bonde la Ziwa Victoria ambayo tayari inashuhudia madhara ya kupungua kwa maji baada ya vituo zaidi ya 1,103 vya maji ya bomba kwa matumizi ya wananchi katika wilaya saba za mkoa huo kukauka na hivyo wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Mkoa huo una zaidi ya vituo vya maji zaidi ya 3,705 kwa ajili ya matumizi ya umma katika maeneo mbalimbali za wilaya za Nyamagana, Ilemela, Kwimba, Magu, Misungwi, Sengerema na Ukerewe lakini vinavyotoa huduma ni 2,379 huku 223 vikihitaji marekebisho.

Akizunguzmia tatizo la maji jimboni kwake, mbunge wa jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula anasema tayari Manispaa ya Nyamagana imepanga kutekeleza mradi mkubwa wa maji utakaogharimu zaidi ya Sh133 bilioni kwa kujenga vyanzo vipya vya maji, kutandaza na kukarabati mitandao na miundombinu ya kusambaza maji kwa wananchi.

“Lengo letu ni kufikia asilimia 90 ya huduma ya maji kwa wananchi ifikapo 2020,” anasema Mabula

Mradi huo pia utahusisha ujenzi wa matanki kwenye maeneo ya vilima kama Isamilo kutakapojengwa tanki lenye ujazo wa lita milioni 1.2 na Bugarika matanki mawili yenye ujazo wa lita 800,000 na lita 200, 000 huku Mkolani ikijengwa tanki la lita 1.2 milioni.

Chanzo: mwananchi.co.tz