Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jinsi lugha zilivyomaliza mauaji ya kishirikina Njombe

Issa Njombe Ed Kamanda wa Polisi mkoani Njombe, Hamis Issa

Thu, 19 Aug 2021 Chanzo: Nipashe

JESHI la Polisi Mkoa wa Njombe limesema limedhibiti mauaji yaliyohusishwa na imani za kishirikina baada ya kuanzisha mkakati wa elimu ikiwamo kumtumia askari polisi anayejua lugha za makabila yote yaliyomo mkoani humo kufikisha ujumbe.

Januari 2019, kulitokea mauaji ya watoto 10 mkoani humo huku miili ya watoto hao ilikutwa ikiwa imekatwa koromeo na sehemu za siri na kusababisha serikali kuunda timu ya uchunguzi.

Katika mahojiano maalum na Nipashe hivi karibuni kuhusu matukio hayo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Hamis Issa, alisema kuwa baada ya kushamiri kwa matukio hayo, Jeshi la Polisi kuanzia Januari mwaka huu liliandaa mikakati mipya ya kuyatokomeza.

“Kilichotokea ni kwamba kila tukio likitokea tulipomkamata mtuhumiwa na kumhoji anakiri kutenda kosa, Jeshi la Polisi tulibaini kuna tatizo la uelewa katika familia na imani za kishirikina zinawafanya wengine kukatishwa uhai," alisema.

Kamanda Issa amesema kuanzia Januari mwaka huu waliweka mkakati maalum wa kutembelea kata kwa kata kutoa elimu kwa wanakijiji inayolenga waachane na imani hizo walizonazo.

“Leo ni Agosti, takriban miezi saba na wiki kadhaa, tumeona mafanikio ya kampeni hii tunayoifanya, matukio ya mauaji ambayo awali yalikuwa yakitokea maeneo mengi Njombe yamepungua," alisema.

Kamanda Issa amesema wanapokwenda kutoa elimu huwa wanaambatana na watu wa dawati la jinsia, dawati linalohusiana na mauaji la mkoa, askari wa usalama barabarani, viongozi wa mila, ustawi wa jamii na viongozi wa maeneo husika.

Amesema kuwa katika utoaji elimu huwa wanazunguka na askari polisi ambaye ana uwezo wa kuongea lugha zote za makabila ya Mkoa wa Njombe ambaye husaidia pale wanaopobaini wanakijiji hawaelewi Kiswahili hasa vijijini.

“Mfano, vijijini tukiwa tunaongea Kiswahili na unaona wanakijiji hawaelewi, hakuna maswali, huyu askari polisi husaidia kuongea nao kwa lugha ya eneo husika, akiongea nao unaona wananchi wanamsikiliza kwa makini mpaka wanatikisa kichwa, hapo tunabaini elimu imewafikia,” alisema.

Kamanda huyo amesema tangu wameanza kutoa elimu, kwa ujumla matukio yamepungua na wanaamini mkakati huo umesaidia na utakuwa endelevu.

“Hata kama mila na desturi ina utata lakini mtu akielimishwa na akaelewa, mfano Mkoa wa Njombe yale matukio ya mauaji ya ovyo ovyo mtu anasema huyu ninamhisi ndiyo amesababisha kifo cha ndugu yangu, huyu ameniroga, yamepungua.

“Yalitokea mara chache maeneo ya Wilaya ya Rudewa lakini wilaya nyingine matukio ya watu kufa ovyo ovyo yamepungua," alisema.

Kamanda Issa amesema matukio yanayotokea ni ya watu kuwasha jiko la mkaa na kulala nayo ndani na wanaendelea kuwaelimisha wananchi athari zake na yale ya watu kujinyonga kwa sababu mbalimbali zikiwamo msongo wa mawazo.

Amesema yale mauaji ambayo yalikuwa yakitokea kwa mtu kudai mzazi wake ndiye amemsababishia umaskini na kumuua kwa sasa yamepungua.

Kamanda huyo amesema elimu hiyo wanayoitoa haijaishia vijijini peke yake kwa kuwa kwa sasa wanakwenda katika maeneo ya mijini ili nao waelimike na kuwaelimisha wengine.

Chanzo: Nipashe