Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jinsi Awadh alivyoyapigania maisha akitumia mtungi wa oksijeni

81001 Awadhi+pic Jinsi Awadh alivyoyapigania maisha akitumia mtungi wa oksijeni

Mon, 21 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Majasiri wengi duniani wanapambana kwa hali na mali kuhakikisha wanapata kile wanachokitaka kwenye maisha. Lakini haikuwa hivyo kwa Hamadi Awadh ambaye alitumia miaka miwili kupigania uhai wake bila ya mafanikio.

Awadh alizikwa jana.

Mwishoni mwa mwaka 2017, Awadh alianza kupata maradhi ya kushindwa kupumua na baadaye mwaka 2018 alianza kuishi kwa kutegemea mashine ya kumsaidia kupumua (oxygen concentrator) baada ya kushindwa kupumua mwenyewe.

Baada ya kutibiwa katika hospitali kadhaa, ikiwemo Hospitali ya Rufaa Amana, Awadh alifikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila Julai 9 mwaka 2018 na kuruhusiwa Julai 9, 2019 baada ya afya yake kuimarika.

Julai 10, Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Mloganzila ilimpa msaada wa mashine hiyo yenye thamani ya Sh4 milioni, kutokana na matatizo hayo ya kupumua.

Tangu aliporuhusiwa kutoka hospitalini Julai 9, alitakiwa kuhudhuria kliniki kila baada ya wiki mbili, jambo ambalo alishindwa kulifanya kwa zaidi ya miezi mitatu kutokana na mazingira magumu aliyonayo.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Septemba 4, Mwananchi ilifanya mahojiano nyumbani kwake Kipawa jijini Dar es Salaam, ambako alitaja changamoto alizokuwa anapitia kimatibabu, kifamilia na kiuchumi.

“Fedha ninayoipata kupitia misaada ya marafiki, inaniwezesha kununua umeme nipumue na dawa na kidogo inayobaki ni chakula cha familia,” alisema Awadh aliyekuwa mjasiriamali Kariakoo kabla ya kupata maradhi hayo mwishoni mwa mwaka 2017.

Alisema gharama za umeme wa kuendesha mashine hiyo ni Sh50,000 kwa wiki na Sh100,000 kwa ajili ya dawa. Alisema dawa hizo huisha ndani ya wiki.

Maelezo yake yaliifanya Tanesco kubeba bili hiyo ya nishati hiyo. Septemba 5, Tanesco ilimfungia umeme katika nyumba aliyokuwa akiishi na kumpa Sh10 milioni za matibabu.

Septemba 11, 2019 Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) lilisema lipo tayari kumlipia gharama za usafiri hadi Mumbai, India ikiwa atapewa rufaa.

Kutokana na changamoto ya usafiri kwenda Mloganzila, Septemba 11 Hospitali ya Aga Khan ilitoa gari la wagonjwa (ambulance) baada ya Awadh kushindwa kuhudhuria kliniki tangu aruhusiwe Juni 9.

Lakini Septemba 12, saa 3:30 gari la wagonjwa kutoka AgaKhan ilifika nyumbani kwake na dakika chache baadaye liliwasili gari la Mloganzila na kumchukua Awadh ambaye alilazwa kwa siku tatu na kuruhusiwa.

Tangu hapo aliendelea na maisha yake mpaka Septemba 23 alipolazwa tena na baadaye kuruhusiwa. Oktoba 4 alilazwa baada ya kupata shinikizo la damu ikidaiwa ni kutokana na kutapeliwa Sh1.05 milioni.

Sakata hilo liliibuka baada ya kununua bodaboda kupitia michango mbalimbali ambayo alikuwa akitumiwa katika simu yake, ambayo baadaye alifikiria kutafuta biashara ili iendelee kumuingizia kipato.

Hata hivyo fedha hizo zilirudishwa kupitia ofisi ya serikali ya mitaa wa Kipawa Oktoba 17, siku ambayo Awadh alifariki.

Mwili wa Awadh ulizikwa jana katika makaburi ya Segerea baada ya kuswaliwa katika msikiti wa Alif Lam Mim uliopo Uwanja wa Ndege ambako uliwasili saa 9:00 alasiri.

Baba mkwe wa marehemu Beneti Kalekana alisema ruhusa ya kuchukuliwa kwa mwili huo ilichelewa kutolewa kwa kuwa walikuwa wanadaiwa “fedha zaidi ya Sh4 milioni na tulikuwa tunadaiwa fedha ya mochwari ya siku mbili. Msamaha wake ulichukua muda,” alisema Kalekana.

Chanzo: mwananchi.co.tz