Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limewataka waendesha pikipiki mkoani humo kuwa na ushirikiano hasa wanapopata abiria wa kutaka kupelekwa maeneo ya nje ya mji ili kuepusha matukio mabaya yakiwemo utekaji na mauaji.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara Nicodemus Katembo amesema kuwa April 24 katika kijiji cha Mnyundo Wilaya ya Mtwara mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Ahmad Saidi Kofi (25) mkazi wa Mikindani ‘alimuua’ Msuko Abrahama Juma (30) dereva wa pikipiki mkazi wa Mikindani kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali tumboni mkono wa kulia.
Katembo alisema kuwa baada ya kutekeleza mauaji hayo mtuhumiwa alimfunga kitambaa shingoni marehemu na kuutupa mwili wake katika pori lililoko katika kijiji hicho.
“Mtuhumiwa alimkodi marehemu kama abiria ili aweze kumpeleka katika kijiji cha Mnyundo na ndipo alipotekeleza mauaji hayo aliondoka na pikipiki ya marehemu aina ya TVS yenye na za usajili MC 299 DRK rangi nyeusi mali ya marehemu”
“Baada ya kuondoka na pikipiki hiyo mtuhumiwa alifika katika kijiji cha Mnyundo na kupeleka pikipiki hiyo kwa rafiki yake aitwae Said ambaye kwa muda huo hakuwepo nyumbani kwake ambapo alikuwa kwa mama ake mzazi”
“Said aliporudi na kuikuta pikipiki ikiwa nje imeegeshwa aliamua kuikokota na kuipeleka kwa mama yake mzazi na mtuhumiwa ambapo taarifa za mtu kuuwawa na kunyanganywa pikipiki zilishafika kijijini hapo jambo ambali lilimfanya mama mzazi wa mtuhumiwa akishirikiana na mtoto wake wa kike kuiondoa pikipiki hiyo na kuitelekeza vichakani”
Hata hivyo wananchi walipoiona waliamua kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambalo liliichukua pikipiki hiyo.
“Baada ya mtuhumiwa kurejea Mikindani, taarifa za kurudi kwake ziliwafikia wananchi na kuamua kwenda kumkamata mtuhumiwa ambaye alikimbia hata hivyo alikamatwa eneo la Mbae na kupelekea kumshambulia kwa mawe na fipo hadi alipofikwa na umauti.
Miili ya marehemu wote wawili ilifanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kukabidhiwa kwa ndugu zao kwa aajili ya maziko.
“Nitoe wito kwa madereva bodaboda wawe makini na watu wanaowakodisha kwenda maeneo ya nje ya mji kwa ni wengi hawana nia nzuri kama kuna ulazima wasindikizane zaidi ya mmoja lakini pia ni vema wananchi wakaacha kujichukulia sheria mkononi” alisema Kamanda Katembo.