Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jina la Sugu lawatesa viongozi Mbeya

49644 SUGU+PIC

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jina la mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu limeendelea kuwasumbua viongozi wa Serikali na kisiasa jijini humo.

Inavyoonekana viongozi hao wanafanya kila linalowezekana kupunguza nguvu zake ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi Mkuu mwakani.

Sugu ambaye amekuwa mbunge wa Mbeya Mjini kwa vipindi viwili sasa ana nguvu kubwa kisiasa zilizompatia kura 108,566 mwaka 2015 na jiji hilo kupata madiwani 36 wa Chadema dhidi ya 10 wa CCM.

Kutokana na hali hiyo imekuwapo mikakati iliyonukuliwa ikielezwa na mkuu wa mkoa huo, Albert Chalamila hivi karibuni, ya kupunguza nguvu hiyo na kuhakikisha wananchi wote ni ‘kijani’ tena. Kijani ni rangi inayotumiwa na CCM katika machapisho na mavazi yao.

Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake hivi karibuni hivi karibuni, Chalamila alieleza mikakati ya kuwaunganisha wananchi ili waachane na siasa zilizochukua nafasi na kusababisha malumbano ya kivyama.

Alielezea kukerwa na jinsi Sugu ama anavyojiita au kuitwa na wafusia wake ‘rais wa Mbeya’ wakati Rais wa nchi yupo, hali aliyosema inatokana na wananchi kuwa na tafsiri potofu ya mfumo wa vyama vingi. “Mbunge usijiite rais, ni kumisbehave (utovu wa nidhamu) na ni uhaini. Hata kama watu wanakuita si ukatae,” alisema.

Mbali na Chalamila, mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika alisema alipofika wilayani humo 2016 hali ya kisiasa ilikuwa mbaya, lakini hivi sasa mambo yanaanza kubadilika na kuwa tulivu.

Akifafanua kauli yake, alisema ilikuwa haiwezekani mtu kuvaa vazi la kijani (sare ya CCM) ila vazi la upande wa pili (Chadema) ndilo lilikuwa linatawala, lakini baada ya kazi kubwa hali imebadilika na nguvu za Sugu zinapungua.

Kauli za viongozi hao zinamwamsha Sugu anayesema wanaosema umaarufu wake umepungua wanajidanganya kwa kuwa wamezuia mikutano ya wapinzani na kuruhusu ya chama kimoja peke yake.

Anahoji kama nguvu zake zimepungua mbona anazuiwa asifanye mikutano na hata kwenda kutoa misaada.Sugu anaeleza pia jinsi suala la yeye kuitwa rais wa Mbeya lilivyoanza na watu waliolianzisha huku akisema yeye hana uamuzi nalo.



Chanzo: mwananchi.co.tz