Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jiji lawabana wafanyabiashara wa mboga, matunda

0e13292dc838c8b7dff38b91f501213f Jiji lawabana wafanyabiashara wa mboga, matunda

Thu, 28 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

OFISA Masoko wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, James Yuna amewataka wafanyabiashara wa matunda na mbogamboga waliopo Stendi ya Daladala ya Sabasaba na kwenye maeneo yasiyo rasmi kuheshimu sheria na maelekezo yanayotolewa.

Alisema hayo jana wakati akizungumza na wafanyabiashara wa mbogamboga na matunda wa stendi ya hiyo pamoja na wanaofanya biashara zao kwenye maeneo yasiyo rasmi ambao wanatakiwa kuhamishia biashara zao eneo lililotengwa na Halmashauri ya Jiji kwenye soko la Makole jijini hapa.

Yuna aliwataka wafanyabiashara hao kutii sheria na maelekezo yanayowataka kuhamia kwenye soko hilo la Makole ambalo limetengwa rasmi na jiji kwa ajili ya utoaji wa huduma muhimu kwa jamii bidhaa za mbogamboga na matunda.

Akizungumza na wafanyabiashara hao ikiwa sehemu ya ziara yake ya kutembelea wafanyabiashara, alisema eneo lililotengwa kwa ajili ya mbogamboga na matunda la soko la Makole, bado kuna nafasi ya kutosha na pia lina vigezo vinavyostahili vya kufanya biashara zao kwa uhuru na kwa misingi na taratibu na sheria zilizowekwa.

“Nataka kuwaambia ndugu zangu wafanyabiashara mnaofanya biashara katika stendi hii ya daladala ya Sabasaba hapa siyo rafiki kwenu hata kama mnajipatia riziki yenu, lakini hapa kuna msongamano wa daladala ni hatari kwenu ninyi na wateja wenu mnaweza kuganyangwa hata na bidhaa zenu pia,” alisema.

Alisema Halmashauri ya Jiji limewatengea soko la Makole na wanatakiwa kuhamia huko na si vingenevyo kwa kuwa liko huru na wanaweza kufanya biashara zao bila kusumbuliwa na magari kama ilivyo Stendi ya Daladala ya Sabasaba.

“Kwanza hapa ni stendi ya daladala na kuendelea kufanyia biashara eneo hili ni kuhatarisha maisha yenu na wateja wenu jambo ambalo haliwezi kuwa sahihi katika uendeshaji wa shughuli za masoko,” alieleza Yuna.

Kwa upande wa wafanyabiashara wa matunda na mboga mboga katika stendi ya daladala Sabasaba, wamesema wapo tayari kuhamia soko la Makole lakini kinachotakiwa ni kuimarisha miundombinu mbalimbali inayohitajika.

Mwanahamisi Omari akizungumza kwa upande wa wauza nyanya stendi ya Sabasaba, alisema kamwe hawako kinyume kwa kubishana na Halmashauri ya Jiji, bali wanachohitaji kuboreshewa miundombinu ili wafanye biashara kwa uhuru na wako tayari kutii maelekezo na sheria na kuhamia kwenye soko la Makole.

“Sisi tupo tayari kuhamia katika soko la Makole na kuondoka katika soko la Stendi ya Daladala Sabasaba lakini tunachoomba wafanyabiashara wengine wa matunda, mbogamboga, nyanya na vitunguu wasibaki humu ndani bali kinachotakiwa ni kuondoka kwenye kwenye hilo soko tulilopangiwa na halmashauri yetu,” alisema Omari.

Mfanyabiashara mwingine, Juma Hamisi alisema tatizo lililopo kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao wanakataa kuondoka na wanabaki huku stendi ya daladala na maeneo mengine yasiyo rasmi, hali ambayo imekuwa ikisababisha wateja walio wengi kutoenda Makole jambo ambalo bado linaweza kuwa gumu kwa upande wao kibiashara.

Chanzo: habarileo.co.tz