Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jiji la Mwanza kujengwa upya

Mwanzaapicc Jiji la Mwanza kujengwa upya

Wed, 30 Nov 2022 Chanzo: mwanachidigital

Wanaliita Jiji la Mawe (Rock City) kutokana na mwonekano wake wa kuzungukwa na milima yenye mawe mengi huku baadhi ya wakazi wakijenga nyumba zao kwenye miamba.

Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka huu yanaonyesha Mwanza ni mkoa wa pili kwa idadi kubwa ya watu ukiwa na zaidi ya watu milioni 3.69 nyma ya Dar es Salaam wenye milioni 5.38.

Sensa hiyo pia imeonyesha Mwanza ni ya pili kwa idadi kubwa ya majengo. Wakati Dar es Salaam ikiongoza kwa kuwa na nyumba 913,707, Mwanza zipo 868,430 na Dodoma836,909.

Hata hivyo, kutokana ongezeko la watu mkoani Mwanza, sura ya jiji imeanza kuharibika kutokana na makazi holela hali iliyolazimu kuandaliwa kwa mpango kabam be wa kulijenga upya jiji hilo kwa ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi (PPP).

Akitoa mada katika Jukwaa la Maendeleo Endelevu (GGP) uliojadili usimamizi madhubuti wa fukwe kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii hivi karibuni, Ofisa Mipangomiji wa Jiji la Mwanza, Evodia Kisoka amesema kutakuwa na maboresho ya ufukwe wa Tampere ambao ni miongoni mwa zinazomilikiwa na Serikali, nyingine ni Kamanga.

Fukwe zinazomilikiwa na watu binafsi mkoani humo ni Faulu, Jembe ni Jembe, Waghill, Rock Beach, Kishimba, Kapricabana, Tamali, Sunset, Shafick Meral na Havash.

Ufukwe wa Tampere

“Ufukwe wa Tampere upo mkabala na jengo la Benki Kuu ya Tanzania ambao unaanzia Mto Milongo na unaambaa hadi kona ya Kirumba. Ukubwa wa eneo ni hekta 9.30,” anasema Kisoka.

Ofisa huyo anasema mpango kabambe (master plan) wa Jiji la Mwanza wa mwaka 2015 hadi 2035 unaonyesha ufukwe wa Tampere utakuwa na jengo kubwa litakalokuwa alama ya Mwanza.

“Katika eneo hilo, maji ya ziwa yatasukumwa na kutengeneza ras ambako kutajengwa jengo refu ambalo ni alama (iconic building) ya utambulisho wa Jiji la Mwanza,” anasema.

Katika eneo hilo, anasema kutakuwa na alama nyingine mbili, kusini kutakuwapo beacon ambayo ni alama ya ufuatiliaji (police patrol and watch tower) na upande wa kaskazini kutakuwa na jengo litakalotambulisha shughuli za majini.

Miradi mingine, Kisoka anasema ni michezo ya watoto, miundombimu kwa ajili ya watu kupumzika, eneo la michezo ya ufukweni na burudani, na mapishi ya samaki kama vile kuoka na kubanika.

Akieleza faida za mradi huo, Kisoka anasema wananchi watapata sehemu nzuri yenye madhari yenye hewa safi kwa ajili ya kupumzika na michezo.

“Kutakuwa na fursa za kiuchumi kwa wajasiriamali na kimazingira, eneo litakuwa na madhari nzuri ya kuvutia,” amesema.

Hata hivyo, anasema kwa muda mrefu maeneo hayo yamekuwa hayafikiki kirahisi kutokana na ubovu wa barabara ndio maana kuna mpango wa kuendeleza fukwe kudhibiti uchafuzi wa mazingira kutokana na utupaji taka ovyo.

Kisoka anasema Halmashauri ya Jiji la Mwanza inakusudia kuingia ubia na sekta binafsi kuuendeleza ufukwe huo.

“Ufukwe wa Tampere unatoa fursa kwa wawekezaji wakubwa, wa kati na wadogo kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza kwa kujenga hoteli, maduka makubwa, ya kati hata ndogondogo.

“Alama ya utambulisho wa Jiji la Mwanza itakuwa kivutio kwa watalii wa ndani na nje. Wakazi wa Jiji la Mwanza na wageni watapata fursa ya kufanya utalii wa ufukweni,” anasema.

Akifafanua kuhusu mpango huo utakaogharimu Sh3 trilioni, Ofisa Mipangomiji wa Mkoa wa Mwanza, Misana Bihemo anasema wakati wanautengeneza waliangalia unakoelekea mji.

“Mwanza imezungukwa na milima ambayo ni kikwazo cha ukuaji wa mji, kwa hiyo inatoa mwelekeo wa kwenda ziwani ndiyo maana tunafanya reclamation (utengenezaji wa rasi) inayotegemea ripoti za mazingira, kama itashindikana itabidi tupunguze miradi kutoka 25 hadi 22,” anasema.

Mpango huo pia unakusudia kuboresha makazi ya wananchi waliopo milimani.

“Hatuwezi kuwa na mpango huu halafu watu waendelee kuwa pale milimani. Unajua hadi mtu anakwenda pale, anakuwa na sababu zake, inawezekana ni urahisi wa usafiri wa kuja mjini. Kwenye mpango huu tutafanya maboresho ya makazi ingawa watu watabaki palepale,” anasema.

Akifafanua kuhusu hilo, Bihemo anasema kwenye eneo la mita za mraba 100 kunaweza kuwa na nyumba 50 hivyo pakijengwa ghorofa patakuwa salama zaidi likipita tetemeko la ardhi.

Bihemo aliyeshiriki kuandaa mpango huo, anasema kuna miradi 25 katika eneo hilo lakini wataanza na mitano ambayo ni kichocheo ili izalishe fedha za kujenga mingine.

Uzoefu wa NSSF

Akizungumza katika eneo litalojengwa mradi huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Profesa Godius Kahyarara ameshauri ushirikishwaji wa kutosha kuepusha mgongano utakaochelewesha utekelezaji.

Profesa Kahyarara aliyewahi kuwa mkurugenzi mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ametoa mfano wa mradi wa nyumba za Dege uliopo Kigamboni jijini Dar es Salaam ambao sasa unatafutiwa mwekezaji mpya.

“Kwa mfano ule mradi wa Dege, sijui kama mliona mpango wake, sasa hivi tunatafuta mteja wa kuja kuununua. Kwa hiyo msichukulie kirahisi, mjue na mwekezaji akija ana matamanio yake. Mtu pesa anayo lakini huu mchoro hautaki, mnafanyaje?” alishauri.

Huku akitoa mfano wa mradi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Profesa Kahyarara pia ameshauri kuwa na miradi kama hiyo haipaswi kuwekwa kiporo inapoanza.

Chanzo: mwanachidigital