Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jiji kusaidia taasisi fedha maeneo yaliyopimwa

8943863df83730f52fd282a3cb222dc1.jpeg Jiji kusaidia taasisi fedha maeneo yaliyopimwa

Wed, 3 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

JIJI la Dodoma mwaka wa fedha 2021/2022 litatenga fedha kwa ajili ya kusaidia taasisi zinazohusika na kufikisha huduma katika maeneo yaliyopimwa ili kuharakisha uwekezaji na uendelezaji wa maeneo hayo.

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru amesema mwaka wa fedha 2021/2020 jiji hilo litatenga fedha kwa ajili ya kuchangia bajeti ya taasisi tatu ili ziweze kufikisha haraka miundombinu ya barabara, umeme na maji katika maeneo yaliyopimwa.

Alisema kwa kuanzia jiji litatenga fedha kwa ajili ya kuchangia bajeti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Duwasa) kwa lengo la kusaidia taasisi hiyo kuchimba visima na ufikishaji wa miundombinu ya maji katika maeneo yaliyopimwa yanayokua kwa kasi.

Mafuru alisema katika mkakati huo, jiji pia litatenga fedha kwa ajili ya kusaidia Wakala wa Usambazaji Maji Vijijini na Usafi wa Mazijingira Vijijini (Ruwasa) ili uweze kufikisha huduma za maji katika maeneo yaliyopimwa kwa haraka.

Alisema pia jiji litatenga fedha kwa ajili ya kusaidia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) ili kuwezesha ujenzi wa madaraja matatu katika eneo la Mji wa Serikali Mtumba.

Mafuru alisema pia jiji litatenga fedha kwa ajili ya ufunguzi wa barabara katika maeneo mbalimbali ya jiji ili kuhakikisha miundombinu hiyo inafunguka na kupitika kwa urahisi wakati wote.

"Jiji litatenga fedha katika bajeti yake kwa ajili ya kuimarisha barabara katika maeneo ambayo kuna mradi mkubwa wa ujenzi wa viwanda ambayo yanafika urefu wa kilometa 112."

"Jiji limeaninisha barabara katika maeneo mbalimbali zenye urefu wa kilomita 112 ambazo inatarajia kuanza kuzifungua," alisema.

Alisema kwa sasa jiji limefanikiwa kufungua barabara katika maneo ya Michese, Iyunbu, Nzuguni na baadhi ya maeneo ya Mtumba na linaendelea na mkakati huo katika maeneo mengine.

Mafuru alisema mkakati wa jiji ni kuhakikisha barabara zote zinafunguka kwa haraka na katika kufanikisha hilo, linaendelea na ukarabati wa mitambo yake minne ili iweze kutumika kutengeneza miundombinu hiyo na kupunguza gharama za kutumia makandarasi.

"Hadi sasa mitambo iliyokamilika na inafanyia kazi ni D5, D6 na greda mbili na pia jiji litanunua mitambo mingine miwili katika bajeti, miwili katika bajeti hii kwa ajili ya kufungua barabara," alisema.

Mafuru alisema maeneo yaliyopangwa kupimwa na kukamilishwa yanayohitaji vipaumbele vya barabara, maji na umeme ni Nala, Michese, Mkonze, Ihumwa na Nkuhungu.

"Maeneo mengine ni Nzuguni, Ndachi, Matuli, Mnadani, Veyula, Msalato, Kikombo, Mtumba na Muhuji," alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz