Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jiji Mwanza lakusanya bil 7/- miezi sita

4b918e60ed842e532cadbc35e386eb9d.jpeg Jiji Mwanza lakusanya bil 7/- miezi sita

Tue, 20 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JIJI la Mwanza limekusanya zaidi ya Sh bilioni saba kutokana na makusanyo ya ndani kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, hivyo kuelekea kuvuka malengo ambayo imejiwekea.

Hayo yamebainishwa jana kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichokutana jijini Mwanza kujadili utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM iliyopitishwa mwaka 2020.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi alisema zaidi ya Sh bilioni 7.2 zimekusanywa toka vyanzo vya ndani.

Makilagi alisema makusanyo hayo ni zaidi ya asilimia 83 ya lengo la kukusanya zaidi ya Sh bilioni 8.6 ambayo eneo hilo lilijiwekea kukusanya katika kipindi cha mwaka 2020/21 ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Aliwataka watendaji wote kufanya kazi kwa juhudi ili watimize malengo yote ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika eneo hilo na kuwaondolea wananchi kero zinazowakabili ili taifa lifikie maendeleo ya ujenzi wa nchi ya viwanda.

Katika kikao hicho, wajumbe walitaka juhudi kubwa kuelekezwa katika kuondoa kero zilizopo katika miradi ya maji na elimu ili wananchi wapate huduma hizo kwa kiwango kikubwa zaidi.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Leonard Msenyele alisema kwa sasa eneo la Wilaya ya Ilemela, Jiji la Mwanza na Kisesa mahitaji yake ya maji ni lita milioni 154 kwa siku huku uwezo uliopo kwa sasa ni lita milioni 90 kwa siku.

Msenyele aliwatoa wasiwasi wajumbe kwa kusema ipo miradi mikubwa iliyoanza kutekelezwa ya ujenzi wa matangi makubwa Butimba itakayozalisha lita milioni 44 na Nyamazobe ambayo kwa pamoja itawezesha uzalishaji wa lita milioni 250 kwa siku.

“Tumeshapata shilingi bilioni 77 kwa ajili ya kujenga tangi kubwa la maji Nyamazobe hivyo tutakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 250 kwa siku, tutatosheleza upungufu wa maji na kuwa na ziada,” alisema Msenyele.

Naye Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba alisema wamejipanga kujenga shule tano mpya za sekondari na vyumba vya madarasa 120 ili kuweza kukidhi mahitaji ya upungufu kwenye eneo hilo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz