Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jiji Dodoma lapitisha bajeti bil 121/-

Ec08c5754e9a33edb288b1eb9edf1935 Jiji Dodoma lapitisha bajeti bil 121/-

Fri, 12 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamejadili na kupitisha bajeti wa Sh 120,841,764,871 mwaka wa fedha 2021/2022 huku asilimia 83 ya fedha hizo zikielekezwa kwenye maendeleo na huduma za kijamii.

Akiwasilisha mapendekezo ya ukomo wa bajeti, Mkurugenzi wa Jiji ambaye pia ni Katibu wa Baraza hilo, Joseph Mafuru alisema fedha hizo zinatoka kwenye vyanzo mbalimbali yakiwemo mapato ya ndani, serikali kuu, wadau wa maendeleo na michango ya wananchi kupita shughuli za maendeleo.

"Halmashauri imepokea ukomo mpya wa bajeti ya miradi itakayotekeleza kwa mwaka 2021/2022 ambayo imebadilisha mapendekezo ya awali ya sura ya bajeti ya halmashauri kutoka makisio ya shilingi bilioni 118.841 na kufikia shilingi bilioni 120.831," alisema Mafuru.

Katika mkutano huo maalumu wa baraza ulioongozwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe, Mafuru alisema jiji limeelekeza nguvu katika maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi yatakayowezesha kuinua na kukuza uchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma,kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja kwa kuwekeza katika miundombinu ya uchumi.

Alitaja maeneo mengine kuwa ni kutoa mikopo, kuimarisha miundombinu, utoaji wa huduma za afya, elimu na maji.

"Tutakuwa na kazi kubwa ya ujenzi wa madarasa, vituo vya afya, zahanati na hospitali ya Wilaya na kuboresha huduma ya maji."alisema Mafuru. Alisema pia bajeti hiyo inaelekeza nguvukuendelea kustawisha makao makuu.

"Pia kazi yetu ya kustawisha makao makuu inaendelea kwa hiyo tuna kazi ya kupanga mji, kupima viwanja na kumilikisha ambayo inakwenda sambamba na kuboresha barabara na miundombinu itakayowezesha watu kuendeleza maeneo yao."alisema Mafuru.

Aidha, alibainisha miradi ya maendeleo ambayo imepangwa kutekelezwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 ni pamoja na kukamilishwa miradi inayoendelea kutekelezwa

"Tuna viporo vingi vya miradi inayondelea kutekelezwa, Kupitia Bajeti hii tunakwenda kukamilishwa viporo na pia kuchangia nguvu za wananchi inapobidi”alisema Mafuru.

Alisema bajeti hiyo pia itekeleza miradi ya maendeleo itakayoleta tija kwa wananchi na ustawi wa Jiji la Dodoma, kuimarisha sekta ya elimu, afya, maji, kuweka mazingira mazuri kwa watumishi na kuimarisha utoaji huduma katika maeneo ya pembezoni

"Tukiimarisha utoaji huduma maeneo ya pembezoni inamaana Jiji letu litakuwa na ukuaji wa pamoja."alsema Mafuru.

Katika Bajeti ya mwaka 2019/2020, Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilipanga kukusanya Sh bilioni 163.29 hadi kufikia Juni 30 mwaka 2020, makusanyo halisi yalikuwa Sh bilioni 126.66 ambayo ilikuwa ni sawa na asilimia 77.3 ya makisio ya bajeti.

Aidha kwa mwaka huo wa fedha makisio ya makusanyo ya ndani ilikuwa ni kukusanya Sh bilioni 59.11, na mpaka Juni 30, 2020 Halmashauri ilikusanya sh bilioni 52.219 sawa na asilimia 88.

Katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2020/2021, hadi kufikia Desemba 30, mwaka 2029, Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilikusanya sh bilioni 41.9 sawa asilimia 24 ya makisio ya kukusanya Sh bilioni 115.929.

Aidha, kwa makusanyo ya ndani, makadilio ilikuwa ni kukusanya Sh bilioni 47.54 huku Sh bilioni 36.208 zikitengea kwa ajili ya miradi ya maendekeo na makusanyo halisi bilioni 15.404 sawa na asilimia 33 ya makisio.

Aidha, wakichangia bajeti hiyo madiwani walisisitiza usimamizi katika ukusanyaji mapato.

Diwani wa Kata ya Chamwino, Jumanne Ndege aliipongeza bajeti hiyo hasa kutokana na asilimia 83 kuelekezwa kwenye maendeleo na kusisitiza usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato ili kufanya utekelezaji uwe wa asilimia 100.

Diwani wa Nzuguni, Malisel Alloyce alisema katika kudhibi upotevu wa mapato ni vyema mashine za kieletroniki zikaongezwa kutoka mashine moja hadi nne katika kila kata.

Diwani wa Kata ya Kilimani, Neema Mwaluko akisisiza haja ya kuwekeza katika elimu na kusisitiza kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa madiwani kuwa wasimamizi wa karibu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz