UJENZI wa Jengo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma ambalo limegharimu zaidi ya Sh bilioni mbili limekamilika na kuanza kutumika.
Akitoa taarifa hiyo mhandisi wa halmashauri hiyo, Ludger Nchimbi alisema ujenzi wa jengo hilo ulianza rasmi mwaka 2017 na kwamba mradi umejengwa kwa awamu tatu.
Alisema katika awamu ya kwanza mkataba ulikuwa unatekelezwa na mkandarasi ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA),ambao uligharimu zaidi ya Sh milioni 493, awamu ya pili ni mkataba wa zaidi ya Sh bilioni mbili na awamu ya tatu ujenzi umefanyika kwa ‘force account’ kwa ajili ya umaliziaji wa mradi huo.
“Tulipokea fedha kutoka serikali kuu Sh bilioni tatu ambazo zimetumika kutoka mapato ya ndani, fedha iliyotumika mpaka kukamilika jengo ni zaidi ya shilingi bilioni mbili,”alisema.
Hata hivyo, mhandisi huyo alisema TBA ilisimamishwa kuendelea na kazi ya ujenzi na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme Juni 6 mwaka huu,baada ya mkandarasi huyo kupata changamoto ya kufungiwa akaunti zake zote na kushindwa kuendelea na kazi, hali iliyosababisha halmashauri kutumia force accoung kukamilisha mradi huo.
Alisema mradi wa jengo hilo kwa sasa umekamilika na tayari umeanza kutumika kuanzia Oktoba 21, 2020.