Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jeneza lazua taharuki Mbeya

90544 Jeneza+pic Jeneza lazua taharuki Mbeya

Thu, 2 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Jiji la Mbeya nchini Tanzania haliishiwi kwa vituko vya ajabu na kuzua taharuki kwa wananchi. Usiku wa kuamkia leo Jumatano Januari 1, 2020 wakazi wa mtaa wa Soweto eneo la soko la samaki wananchi wamekumbwa na taharuki baada ya kuamka na kukuta jeneza tupu likiwa limewekwa nje ya moja ya duka.

Tukio hilo ambalo linahusishwa na imani za kishirikina limeacha maswali mengi kwa wafanyabiashara wa samaki na wananchi wengine waliofika eneo hilo na kushuhudia jeneza hilo likiwa limetelekezwa huku likionekana limefukuliwa toka kaburini.

Kutokana na tukio hilo, Polisi mkoani Mbeya linamshikilia mtu mmoja kuhusiana na tukio hilo huku likiendelea na uchunguzi wa kina ikiwa ni kubaini mahali lilipotoka jeneza hilo na lengo la kwenda kulitelekeza eneo hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amesema, “tunaendelea na uchunguzi ili kubaini sababu za jeneza hilo kutelekezwa sokoni hapo. Wakati tukiwa tunamshikilia mtu mmoja kuweza kusaidia upelelezi wetu.”

Mmoja wa wafanyabiashara wa samaki eneo hilo, Oscar Kilasi amesema kitendo cha kudamka asubuhi kuwahi kufungua biashara yake na kukuta tukio hilo limewaacha na maswali yasiyokuwa na majibu ya harakaharaka kwani sio kawaida eneo hilo kukumbwa na matukio ya ajabu kama hilo.

“Nimewahi kuja ili kufungua biashara yangu nikiamini leo sikukuu ya mwaka mpya wateja watahitaji kujipatia huduma asubuhi asubuhi, lakini nilichokutana nacho ni ajabu kabisa. Nimekuta mbele ya duka la jirani yangu kwenye meza juu kuna jeneza kubw,” amesema

Amesema ana amini vyombo vya dola vitafanya kazi yake ili kubaini ukweli wa jeneza hilo kuwekwa eneo hilo na kusababisha taharuki kubwa kwao (wafanyabiashara), wateja wao lakini wananchi kwa ujumla wa jiji hilo.

Mwenyekiti wa Soko la Soweto, Fred Mwaiyongano amesema baada ya kuliona jeneza hilo alianza kufuatilia kwa kina ili kujua limefikaje sokoni hapo kwa sababu sio tukio la kawaida ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na vijana ambao huwa wanafanya kazi ya kushusha mizigo eneo hilo kila siku.

“Wamenieleza kwamba jeneza hilo lilishushwa sokoni hapo na lori aina ya Fuso lililokuwa limeleta nyanya likitokea Makambako mkoani Njombe.”

Alisema baada ya kuambiwa hivyo, walifanya mawasiliano watu wa kupakia mizigo kutoka Njombe, ambao walimueleza jeneza hilo lilisafirisha mwili wa marehemu kutoka Mbeya kwenda Makambako na lilitakiwa kurudishwa Mbeya.

Alisema watu walilipakia katika gari lao kwa lengo la kulipeleka kwenye mmoja wa Msikiti uliopo Sokomatola jijini Mbeya, lakini dereva akaliacha sokoni hapo badala ya kulifikisha eneo husika.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Soweto, Ramadhan Tavee amesema tukio hilo limewashtua wananchi wake kwa vile sio la kawaida na kwamba kinachoshangaza zaidi limetelekezwa mbele ya duka ambalo mmiliki wake anauguza mgonjwa hospitalini.

Chanzo: mwananchi.co.tz