Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jamii yatakiwa kuwajengea uwezo walemavu

Fri, 7 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jamii imetakiwa kuachana na dhana potofu kuwa walemavu wanahitaji huruma na msaada wa fedha na badala yake wawajengee uwezo ili waweze  kujitegemea.

Akizungumza katika siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu iliyokwenda sambamba na huduma ya upimaji afya bure kwa watu wa kundi hilo iliyotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo, mkurugenzi wa kampuni ya Compass, Maria Sarungi alisema jamii inapaswa kuacha kuwaona walemavu kama watu wanaohitaji kusaidiwa siku zote.

“Ifike wakati utu wa mtu mwenye ulemavu uthaminiwe,  hawahitaji kuonewa huruma tu, huruma inapaswa kuambatana na kumwezesha ili aweze kujitegemea na kuishi bila msaada wa mtu, ” alisema.

Naye mkurugenzi wa asasi ya Maisha ya Amani kwa watu wenye ulemavu,  Sophia Mbeyela alisema watu wa kundi hilo wana uwezo mkubwa hivyo wapewe nafasi ya kuonyesha walivyonavyo.

“Siku zote nimekuwa nikiamini walemavu tunaweza na ninaendelea kusisitiza kuwa mlemavu haina maana uwe ombaomba, akili iko sawa itumie ili uonekane mchango wako na umuhimu wako kwenye jamii,” alisema Mbeyela.

Maadhimisho hayo ambayo hufanyika Desemba 3 kila mwaka duniani kote, mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu ‘Tuwajumuishe, tuwashirikishe na tuwapatie haki sawa watu wenye ulemavu.’



Chanzo: mwananchi.co.tz