Handeni. Ili kuimarisha elimu jumuishi nchini Tanzania jamii imetakiwa kuwafichua watoto wenye ulemavu kuanza madarasa ya awali kama ilivyo kwa watoto wengine.
Mshawishi na Mtetezi wa Shirika la Kimataifa la ADD Intenational linalojishughulisha na watu wenye ulemavu, Asteria Gwajima amesema hayo leo Jumanne Mei 28, 2019 wakati akizungumza katika juma la elimu linalofanyika wilayani Handeni chini ya uratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Ten/Met).
Gwajima amesema msingi wa elimu kwa kila mtoto ni elimu ya awali lakini baadhi ya wazazi na walezi huwaficha watoto wao mpaka umri wa kuanza darasa la kwanza.
"Kama mtoto mwenye ulemavu atakosa msingi wa awali haitakuwa sawa, jamii lazima iwafichue hawa watoto," amesema Gwajima.
Awali Mdhibiti ubora wa kazi za shirika la Haki Elimu, Robert Mihayo amesema elimu jumuishi ni ile inayowaunganisha watoto walemavu na wasio na ulemavu kuondoa unyanyapaa.
"Kinachotakiwa na shule kuwa na miundombinu stahiki, watoto wanaposoma pamoja unyanyapaa unaondoka na wote hupata elimu kwa usawa jamii, Serikali na mashirika tunapaswa kufanya kazi pamoja," amesema Mihayo.
Pia Soma
- Utouh ‘alibip’ Bunge, adai halisimamii mapendekezo ya CAG
- Magufuli atua Zimbabwe
- Utaratibu Mkoa wa Arusha kuondoa sokoni mifuko ya plastiki huu hapa
"Kazi ya kuimarisha elimu sio ya Serikali peke yake hili ni jukumu la kila mmoja, mashirika yasiyo ya kiserikali mnajukumu hili pia," amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe amesema wilaya hiyo ni kati ya zile zilizoweka msisitizo elimu jumuishi.