Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jamii isikate tamaa kupinga vitendo vya udhalilishaji wanawake

32361 Pic+jamii Tanzania Web Photo

Wed, 19 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ndoa za kidini na kisheria hutarajiwa kuwa ni mkataba wa mke na mume wa kuishi kwa wema.

Watu wanayo mitazamo tofauti kwa suala la ndoa. Hii hutegemea elimu, upeo wa kuilewa dunia na kwa kiasi gani huyo mtu anayaelewa mafunzo ya dini na mtazamo wake kwa mujibu wa mila na utamaduni wake.

Imani za dini nyingi na sheria za kimataifa sio mume wala mke mwenye haki ya kumdhalilisha au kumnyanyapaa mwenzake.

Jamii nyingi zimechukua hatua za kutoa elimu ya kukataa udhalilishaji na kuwachukulia hatua wanaofanya hivyo.

Hivi karibuni watu wa Zanzibar waliungana na wenzao duniani kote kwa kuwa na harakati tofauti kwa siku 16 kupinga aina zote za udhalilishaji wa kijinsia.

Miongoni mwa yaliyojitokeza ni kuwataka akina mama kutoogopa kutoa taarifa za udhalilishaji wanaofanyiwa.

Ukiangalia juu juu utaona huu ni ushauri sahihi na unaweza kusaidia kumaliza au kupunguza kadhia hii inayowakumbuka wanawake.

Changamoto kubwa ni uelewa mdogo wa raia na hasa akina mama kuhusu haki zao, ikiwa ni pamoja na maisha ya ndoa.

Wapo wanaodai na wapo wanaoamini kwamba mke anao wajibu wa kuridhia lolote atakalo au analolifanya mume kwa mkewe.

Ni kweli zipo sheria zinazomsaidia mwanamke asidhalilishwe, lakini tukumbuke wanawake wanahofia kupewa talaka.

Hii sio kwa sababu ya kumpenda mume bali kuona kuwa mjane ni kujitwisha mzigo usiobeba na sio rahisi kuutua ukisha ubeba.

Wengi huona anapokuwa mjane kazi ya kulea watoto inakuwa ngumu kwa vile wamekuwa wakiwategemea zaidi baba wa hao watoto kutoa mchango mkubwa.

Hapana ubishi zipo sheria zinazomsaidia mwanamke aliyepewa talaka kupunguza mzigo wa ulezi wa watoto, lakini utekelezaji wake una matatizo, hasa ikiwa mume hana kipato kinachoweza kudhibitiwa kirahisi.

Jamii nyingi nazo hazina mtazamo mzuri kwa mwanamke mjane, kama vile ni mtu aliyepoteza sifa ya utu wake na kustahili kuheshimiwa.

Ni vizuri mpango mzuri wa elimu ya kuukataa udhalilishaji wa kijinsia na mwingine ikapewa mkazo zaidi katika shule zetu.

Tukumbuke wasia wa wazee usemao….Udongo upate ulimaji kwani wakati huo ndio inakuwa rahisi kuufinyanga utakavyo na sio wakati ukiwa mkavu kama jiwe.

Watu wengi wanaohudhuria mikutano, semina na makongamano yanayozungumzia udhalilishaji wa kijinsia ni wa umri mkubwa na wameshaupokea udhalilishaji kama jambo la kawaida.

Kuwataka wabadilike ni vigumu. Njia nzuri ni elimu kupewa umuhimu katika shule zetu.

Hata hivyo, mpango huu unahitaji uangalifu. Sio sahihi kutoa elimu hii kwa chekechea au watoto wa chini ya umri wa miaka 12 kwa vile taabu kuelewa mambo ya ndoa.

Kwa hivyo elimu ya ndoa, kukataa udhalilishaji, watu kujua haki zao makazini na katika jamii itolewe kwa mpango maalumu.

Kwa mfano maswala ya ndoa yatolewe maelezo kwa wanafunzi wanaokaribia kumaliza elimu ya msingi na katika shule za sekondari, lakini kwa lugha inayokubalika kwa kutilia maanani utamaduni wa jamii husika.

Tukifanya hivyo tutafinyanga kizazi kitakachokuwa na maisha ya ndoa ya watu kuheshimiana na kushirikiana.

Tusikate tamaa. Tupo safarini kupinga udhalilishaji na tukaze kamba kulimaliza tatizo.



Chanzo: mwananchi.co.tz