Raia wa Uswisi na mpenziwe raia wa Kenya wameshtakiwa kwa kushindwa kulipa ada ya gesti walikokaa kwa zaidi ya miezi mitatu.
Sergio Joao Manuel alishtakiwa pamoja na mpenziwe Pauline Mwende kwa kushindwa kulipa Sh234,000.
Hata hivyo wawili hao walioshtakiwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Lucas Onyina waliomba fursa wasuluhishe kesi hiyo nje ya mahakama.
“Naomba hii mahakama itupe wiki moja tulipe pesa tunazodaiwa na mmiliki wa gesti ambayo tumekuwa tukiishi na Joao. Niko na mtoto wa umri wa miaka miwili ninayemtunza na nikizuiliwa atateseka,” Mwende alimshihi Bw Onyina.
Mshtakiwa huyo alisema watu wa familia yake wanaendelea kusaka pesa hizo kwa udi na uvumba wamlipe mwenye gesti katika eneo la Ngara jijini Nairobi.
Joao alieleza mahakama alikuwa amefika nchini kukutana na mpenzi wake Pauline Mwende.
Raia huyo wa kigeni alisema alikuwa amepanga kuishi na mwende kwa muda wa miezi saba akiweka mipango kamili ya maisha yao ya usoni.
Hakimu aliwaachilia kwa dhamana Sh80,000 pesa tasilimu kila mmoja.
“Mtafika mbele ya hakimu mkuu Februari 21, 2023 kesi hii itengewe siku ya kusikilizwa,” aliamuru Bw Onyina.
Kwa sasa Mwende na Joao waliamriwa wawasiliane na mwenye gesti wasuluhishe suala hilo la renti.
Hakimu aliamuru upande wa mashtaka uwakabidhi washtakiwa nakala za ushahidi wajue jinsi watakavyojitetea.