Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jamaa atiwa mbaroni kwa kuchoma moto nyumba ya mpenzi wake

Pingu Law Jamaa atiwa mbaroni kwa kuchoma moto nyumba ya mpenzi wake

Wed, 20 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Polisi Mkoa wa Mwanza inamshikilia Mkazi wa Buhongwa, jijini hapa Nestory John kwa tuhuma za kuchoma moto nyumba ya mpenzi wake, Eva Stephano na kusababisha vifo vya watu watatu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 20,2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema John (52), anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 7, 2023 katika Mtaa wa Lwanhima jijini hapa.

Mutafungwa amesema mtuhumiwa baada ya kuchoma moto nyumba na kusababisha vifo, akidai ni kutokana na wivu wa mapenzi alitoroka na kukimbilia kwa mganga wa jadi kwa lengo la kuaguliwa ili asikamatwe.

“Baada ya msako mkali, Desemba 16, 2023 saa 10.10 jioni Polisi ilimkamata mtuhumiwa nyumbani kwa mganga wa jadi, Samson Mwinamila mkoani Geita, akioshwa dawa ili asikamatwe na jeshi hilo,” anasema Kamanda Mutafungwa.

Amesema baada ya kumkagua mtuhumiwa walimkuta ana jeraha usoni lililotokana na moto huo wa mafuta, jambo linaloashiria huenda alilipata baada ya nyumba kulipuka.

Wakati huohuo, Kamanda Mutafungwa amesema polisi inamshikilia mkazi wa Dar es Salaam, Elizabeth Ndakubegi (35) na mkazi wa Igoma jijini Mwanza, Farida Masaba kwa tuhuma za kumuua kwa kumchinja mkazi wa Nyamhongolo wilayani Ilemela, Flora Philimon (42).

Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha mauaji yaliyotokea Desemba 14, 2023 yalichangiwa na mgogoro wa mali. Inadaiwa watuhumiwa walipanga njama na kutekeleza mauaji ya wifi yao Flora.

“Baada ya uchunguzi wa kina na ushahidi kukamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani,” amesema.

Katika hatua nyingine, Kamanda Mutafungwa amesema mkazi wa Kagera wilayani Ukerewe, Agrey Mchanga, ambaye ni mtoto amefariki dunia Desemba 18, 2023 kwa kugongwa akiwa amejipumzisha chini ya uvungu wa gari.

“Mtoto huyo anadaiwa kuiacha familia yake na kwenda kuishi na kufanya kazi mtaani baada ya wazazi wake kutengana. Aliamua kupumzika chini ya uvungu wa gari ambalo lilimkanyaga na kufariki dunia,” amesema.

Amesema mwili umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe. Amewashauri wazazi na walezi kuepuka migogoro katika mahusiano na ndoa ili kuwalinda watoto dhidi ya madhara yanayoweza kuwapata, ikiwamo kukosa maadili na vifo kwa kukosa uangalizi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live