Mwanaume mmoja ambaye jina lake halijafahamika amejinyonga na kufariki dunia ukweni kwake baada ya juhudi za kupanisha na mke wake kugonga mwamba.
Mwanaume huyo alikuwa amekwenda ukweni kwake Kijiji cha Kolondo Mashariki mwa Homa Bay, ambapo inaelezwa lengo lake ilikuwa ni kumrudisha mke wake aliyekuwa amerudi kwa wazazi wake kutokana na mtafaruku wa kifamilia.
Hata hiyo, mwanaumkwe huyo alijinyonga baada ya kuona juhudi za kupatanishwa na mke wake ambaye walitengana zigonga mwamba.
Taarifa zinasema kuwa awali, mwanaume huyo aliamua kuondoka na kwenda kusikojulikana, lakini baadaye alirejea usiku kimyakimya nyumbani hapo ukweni kisha kujinyonga.
Chifu wa eneo hilo, Perez Okoth amethibitisha kutokea tukio hilo, akisema mwili wa mwanaume huyo ulikutwa ukining'inia kwenye mti ulioko karibu na nyumba ya mama mkwe wake Jumapili, Machi 12 asubuhi.
"Baada ya kutofautiana na mkewe ambaye alirudi nyumbani kwao, aliamua kumfuata ili kusuluhisha tofauti hizo ili waweze kuungana tena kama familia. Hata hivyo mazungumzo yalionekana kugonga mwamba," imeelezwa.
Siyo tukio la kwanza kulingana na maelezo ya wanakijiji. Tukio hilo ni la pili kuripotiwa katika nyumba hiyo. Inadaiwa kuwa mwanaume mwingine pia aliwahi kujitoa uhai nyumbani humo katika hali kama hiyo.
Chifu wa eneo hilo hata hivyo alitoa wito kwa familia kutafuta njia mwafaka za kutatua masuala ya kifamilia ili kuepukana na matukio kama hayo.
Mwili wa marehemu ulipelekwa mochwari katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Rachuonyo kusubiri uchunguzi wa polisi.