Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jaji mfawidhi Tanga kuwania nafasi ya ujaji Mahakama ya Afrika

10221 Jaji+pic TZW

Fri, 29 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iwapo atachaguliwa, atakuwa Jaji wa pili Mtanzania kuchukua nafasi hiyo baada ya Jaji Augustino Ramadhani

Arusha. Serikali ya Tanzania imempendekeza Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Imani Aboud kuwania nafasi ya kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu (AfCHPR) katika uchaguzi unaofanyika kesho, Mauritania.

Taarifa ya Mahakama hiyo iliyotolewa juzi kwa vyombo vya habari imesema viongozi wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) watawachagua majaji wanne kuziba nafasi zilizoachwa wazi.

Mahakama hiyo yenye jumla ya majaji 11, hutumia utaratibu wa mgawanyo wa kanda tano huku kila kanda ikipata majaji wawili kwa kuzingatia jinsia baada ya nchi husika kuwapendekeza na uchaguzi hufanywa na marais wa AU.

Jaji Aboud anatarajiwa kuchuana na Jaji Lydia Mugambe Ssali wa Uganda ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Salomy Bossa wa Uganda aliyechaguliwa kuwa jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) nchini Uholanzi mwaka jana.

Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fatma Karume alisema anamtakia kila la kheri Jaji Aboud katika uchaguzi huo na anaamini uzoefu wake katika fani ya sheria utamwezesha kuchaguliwa.

“Nimtakie kila la kheri mheshimiwa Imani Aboud, naamini watauona ubora wake na kumchagua aiwakilishe nchi yetu katika chombo hicho kinachosimamia haki za binadamu Afrika,” alisema.

Iwapo atachaguliwa, atakuwa Jaji wa pili Mtanzania kuchukua nafasi hiyo baada ya Jaji Augustino Ramadhani ambaye baada ya kustaafu alichaguliwa kuwa makamu wa Rais wa Mahakama.

Kanda ya nchi za Afrika Magharibi ina wagombea watano ambao ni Jaji Stella Anukam wa Nigeria, Jaji Eliane Egue-Adote wa Benin, Jaji Saran Diakite Keita wa Mali, Jaji Naceesay Salla-Wadda wa Gambia na Jaji Fatimata Toure wa Burkina Faso wanawania nafasi ya Jaji El Hadj Guisse wa Senegal aliyemaliza muda wake.

Kwa upande wa nchi za Afrika ya Kati nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Gerald Niyungeko wa Burundi anayemaliza muda wake inawaniwa na majaji Blaise Tchikaya wa Congo pamoja na Jaji Pacifique Manirakiza wa Burundi.

Chanzo: mwananchi.co.tz