Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jaji Ramadhani kuchangisha fedha za kuboresha Chuo cha St Mark’s

Sat, 20 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa kamati ya kuchangisha fedha za kuboresha majengo ya Chuo cha St Mark's kilichopo Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam, Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhan amewataka wadau mbalimbali kusaidia harambee ya zaidi ya Sh800 milioni kwa ajili ya uboreshaji wa majengo ya chuo hicho.

Jaji Ramadhan amesema hayo leo AlhamisI Oktoba 18, 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari chuoni hapo ambapo amesema uboreshaji wa majengo umekuja baada ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuwataka wafanye hivyo.

Hivi karibuni, TCU ilisitisha utoaji wa mafunzo kwa vyuo vitano na kuamuru wanafunzi wote wanaoendelea na mafunzo katika vyuo hivyo  kuhamishiwa vyuo vingine na kuzuia udahili kwa vyuo saba katika ngazi zote kutokana na kukosa sifa ya utoaji wa elimu ya juu na miongoni mwa vyuo hivyo ni pamoja na St Mark's.

“Nimewaiteni hapa waandishi wa habari nikiwa na lengo la kutaka kutusaidia kuutangazia umma kuwa siku ya Jumamosi Oktoba 20, 2018 tutakuwa na harambee kwa ajili ya kuchagisha fedha za kuboresha majengo yetu kama tulivyoagizwa na TCU" amesema.

Amesema  harambee hiyo itafanyika chuoni hapo kuanzia saa nane mchana na mgeni rasmi anatarajia kuwa Spika wa Bunge Job Ndugai na kwamba TCU iliwataka wafanye ukarabati wa majengo ya chuo hicho.

Amesema zaidi ya Sh800 milioni zinatarajiwa kuchangishwa katika harambee hiyo ikiwa ndiyo fedha ambayo inatakiwa ili kuwezesha uboreshaji wa majengo hayo na kuwataka wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi ili kuwezesha kupatikana kwa fedha hizo.

Chanzo: mwananchi.co.tz