Dodoma. 'Nakupenda, unanipenda, usinishike mkono' ni kampeni inayoanzishwa na Waziri wa nchi ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Seleman Jafo ili Watanzania waache kushikana mikononi.
Jafo amesema hayo leo Ijumaa Novemba 23, 2018 wakati akitoa neno la shukrani kwa hotuba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akifunga semina ya siku tatu kwa maofisa afya wa halmashauri na mikoa nchini iliyofanyika jijini Dodoma.
"Hii ni hatari sana hasa kwa viongozi, utakuta katika mkoa unaofanya ziara watu zaidi ya 40 wanakusubiri mnapeana mikono wakati kuna magonjwa ya kuambukiza, nataka tuwe tunapungiana mikono," amesema Jafo
Amesema viongozi ndiyo watakuwa waathirika namba moja kwani wanaokaa kwenye foleni hizo huwa wametoka maeneo mbalimbali bila kunawa lakini wanakimbilia kuwapa mikono viongozi.
Waziri huyo amesema tayari ameshazungumza na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ili waone namna bora ya kuliweka jambo hilo kwa faida ya Watanzania.
Katika hatua nyingine, Jafo amesema watakaa pamoja na Waziri Ummy ili kupunguza mambo mengine ambayo yanatokana na mambo yasiyo ya lazima.