Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jafo asema vituo vya mabasi vitenge maeneo ya wamachinga, bodaboda

11426 Jafo+pic TanzaniaWeb

Sat, 11 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Waziri wa Tamisemi  Suleiman Jafo  amesema kuanzia sasa vituo vyote vya kisasa vya mabasi vitakavyojengwa nchini ni lazima vitenge maeneo kwa ajili ya wamachinga, bodaboda na mamalishe.

Jaffo ameyasema hayo leo Agosti 11,2018 katika viwanja vya kituo kikuu cha mabasi mjini Moshi, wakati akimnadi mgombea udiwani  kata ya Mawenzi kwa tiketi ya CCM, Apaikunda Naburi.

"Tunapojenga stendi za kisasa kuanzia sasa ni lazima ramani zake zionyeshe Machinga watafanyia biashara zao wapi. Ni lazima zionyeshe mama ntilie watakuwa wapi na bodaboda wataegesha wapi pikipiki zao," amesema.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, hata kituo kipya kikubwa na cha kisasa cha Ngangamfumuni cha mjini Moshi kinachojengwa na Serikali kwa zaidi ya Sh20 bilioni kitakuwa na huduma hizo.

"Hata vituo vipya vya Magomeni na Kisutu Jijini Dar es Salaam na Msamvu mkoani Morogoro tumesema hilo ni sharti mojawapo muhimu. Ni lazima kuwe na mazingira rafiki kwa makundi hayo kufanya biashara,".

Ameongeza kuwa Serikali chini ya Rais John Magufuli itatekeleza na kutatua kero zote katika kata hiyo ya Mawenzi kabla ya 2020 na kusema Apaikunda ndio atakuwa kiungo sahihi kati ya wananchi na Rais.

Amesema katika kipindi hicho, Serikali itahakikisha inaboresha huduma za hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi na kudokeza kuwa katika mwaka 2018/2019, Serikali itajenga hospitali mpya 65 kutoka 77 zilizopo sasa nchi nzima.

Akiomba kura katika mkutano huo, Apaikunda amesema endapo wananchi watampa ridhaa ya kuwa diwani wao, atahakikisha hospitali ya Mawenzi inaboreshwa na Machinga wanajengewa mazingira mazuri ya kufanya biashara.

Awali katibu wa CCM mkoa Kilimanjaro, Jonathan Mabhia amesema, wananchi wa kata hiyo na ile ya Makanya wilayani Same, wamewaahidi kuichagua CCM kwa vile hawaoni chama mbadala.

Katika uchaguzi huo utakaofanyika kesho, Apaikunda atachuana na mgombea wa Chadema, Afrikana Mlay na wa chama cha Sauti ya Umma (Sau), Issack Kireti.

Chanzo: mwananchi.co.tz