Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jafo akerwa kasi ya ujenzi barabara Mji wa Serikali

3311cd1ae396333e8048c85bddc8e96d Jafo akerwa kasi ya ujenzi barabara Mji wa Serikali

Thu, 4 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo ameoneshwa kutoridhishwa na na kasi ya ujenzi wa barabara za Mji wa Serikali Mtumba kwa kiwango cha lami.

Aidha ameagiza mradi huo kukamilika kabla ya Julai 31 mwaka huu.

Akizungunza jana jijini hapa wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo, Jafo alisema hajaridhishwa na utekelezaji wa mradi huo ambao unasuasua kutokana na kuadimika kwa saruji aina ya 32.5N.

Kutokana na changamoto hiyo, Jafo alimshauri mkandarasi kuangalia namna ya kutumia saruji aina ya 42.5N na kufanyiwa vipimo maabara kuangalia namna wanavyoweza kupunguza ili itumike kumalizia barabara.

"Sijaridhishwa na kasi hii maana upo chini kwa asilimia sita kwa maana hiyo sihitaji mjadala wa aina yoyote hapa, nataka ifikapo Julai 30 mradi ukamilike kwa asilimia 100,”alisema.

Jafo alisema kuwa haiwezekani mradi kuchelewa wakati kuna saruji ambayo endapo vitu vikipunguzwa inaweza kutumika katika eneo la ukubwa huo wa saruji inayohitajika.

Awali, akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya mradi, Mkurugenzi wa Barabara Mjini, Mohammed Mkwata alisema hadi kufikia mwishoni mwa Februari mwaka huu utekelezaji umefikia asilimia 63 dhidi ya asilimia 69 kwa mujibu wa mpango wa kazi wa mkandarasi.

"Kuna pengo la asilimia sita dhidi ya mpango na sababu zilizochangia kuwepo kwake ni uhaba wa saruji katika kipindi cha kuanzia Novemba 26 mwaka 2020 hadi Februari 2021 ambapoa waliomba usaidizi kutoka ofisi ya Waziri Mkuu katika kukabiliana na changamoto hiyo.

"Katika kipindi hicho mkandarasi hakuweza kupata saruji aina zote 32.5N na 42.5N kwa kadiri ya mahitaji halisi hali ambayo iliathiri kazi za ujenzi wa vivuko na ujenzi wa tabaka la kwanza la barabara ambalo nalo linahitaji saruji,"alisema.

Mkwata alisema ili kurejea kwenye mpango wa kuwezesha mradi huo kukamilika ifikapo Julai 31 mwaka huu mkandarasi ameongeza mtambo mwingine wa uzalishaji kokoto, zege na lami.

Alisema pia amegawa kazi za mifereji na kwa kampuni ya kizalendo kwa utaratibu maalumu na mkandarasi ametakiwa kuanza zamu za usiku mara moja hali ya upatikanaji wa saruji itakaporejea kwa kiwango cha kuridhisha.

Mkwata alisema Tarura kupitia Mhandisi mshauri itaendelea kusimamia mradi huu kwa karibu zaidi ikiwa ni pamoja na mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana ili kuona kuwa mradi unakamilika kwa muda uliopangwa.

Aidha akikagua ujenzi wa barabara ya mita 200 inayoingia katika hospitali ya Uhuru iliyoko Wilaya ya Chamwino, Jafo alionesha kuridhishwa na ujenzi na kutaka barabara hiyo kukamilika Machi 14 mwaka huu.

Awali, alitoa taarifa za mradi, Maneja Tanroads Chamwino, Nelson Maganga alisema maendeleo ya jumla ya utekelezaji yamefikia asilimia 85 na tayari lami nyepesi imekamilika tayari kwa kuweka tabaka la lami nzito Machi 5, 2021 na kwamba unatakiwa kukabidhiwa Machi 14.

Chanzo: www.habarileo.co.tz