Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JPM akutana na familia ya kijana aliyeuawa Tunduma

F055fae4e0e9de0d6fb67f2617dc8ba1 JPM akutana na familia ya kijana aliyeuawa Tunduma

Sat, 3 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

RAIS John Magufuli amekutana na familia ya kijana Briton Mollel (26) aliyeuawa baada ya kushambuliwa katika vurugu zilizotokea wakati wa urejeshaji wa fomu za kugombea udiwani kwa msimamizi wa uchaguzi wa Kata ya Kaloleni katika Jimbo la Tunduma mkoani Songwe.

Magufuli ambaye aliwasili Mjini Unguja (Zanzibar) jana, pia alimtembelea na kumjulia hali Hamis Nyange Makame (63) aliyelazwa katika Hospitali ya Mnazi mmoja akitibiwa majeraha baada ya kushambuliwa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni wakati akiswali msikitini huko Kangagani, Wilaya ya Wete (Pemba).

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa ilisema Rais Magufuli alikutana na mama wa marehemu, Roda Mwaisongole na mjane wa kijana huyo, Salome Mayao Mjini Tunduma kuwapa pole na kutoa ubani wa Sh milioni sita.

Magufuli amelaani mauaji hayo yaliyofanyika Agosti 25 mwaka huu na ameagiza hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wote waliohusika . Pamoja na familia ya marehemu, alifanya sala fupi ya kumuombea apumzike kwa amani.

Briton ambaye alikuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alimsindikiza mgombea udiwani wa CCM katika kata ya Kaloleni wakati wa urejeshaji wa fomu siku ya tukio.

Ameacha mke na watoto watatu wenye umri wa kati ya mwaka mmoja na miaka 6. Akiwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja ambako alimjulia hali Makame, Rais Magufuli ameagiza vyombo vya dola kuchukua hatua zinazostahili kwa wote waliohusika.

Makame ambaye ni mwana CCM, alishambuliwa Septemba 22 mwaka huu.

Wakati huo huo, Katibu wa Idara ya Itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amelitaka jeshi la Polisi kukamilisha upelelezi na kuwafikisha mahakamani watu waliohusika katika tukio la kushambuliwa kwa mapanga viongozi watatu wa chama hicho Pemba mwezi uliopita.

Chanzo: habarileo.co.tz