Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Iringa yajipanga kufaulisha la saba kwa asilimia 80

Tue, 4 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa. Jumla ya watahiniwa 26,060 katika mkoa wa Iringa wanatarajia kufanya mtihani wa kumaliza darasa la saba kuanzia kesho Septemba 5-6, 2018. Kati ya watahiniwa hao wavulana wakiwa 12,281 na wasichana 13779.

Akizungumza leo ofisini kwake, ofisa elimu wa mkoa wa Iringa, Majuto Njanga amesema maandalizi yapo vizuri ikiwamo usalama upo wa kutosha katika halmashauri zote za mkoa huo.

Amesema tayari mitihani imeanza kusambazwa katika halmashauri za Iringa, kuanzia leo asubuhi kwa sababu usafiri wa mitihani na wasimamizi upo.

“Tumeanza kusambaza mitihani kwenda kwenye vituo, pia usafiri wa kupeleka wasimamizi kusimamia mitihani katika vituo upo na shule zitakazofanya mitihani ni 498,”amesema.

Njanga amesema kama mkoa wanatarajia kufaulisha kwa zaidi ya asilimia 80 na hawatarajii matokeo chini ya hapo kwa sababu wana uhakika wamewafundisha wahitimu vya kutosha.

“Mkoa umejipanga kufaulisha na kupata matokeo si chini ya asilimia 80 kwa sababu tumewaandaa wahitimu vizuri kulingana na mitaala yetu ya elimu na kulingana na masomo kama ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyosema,” amesema.

Amesema hakutakuwa na udanganyifu wa mitihani kwa sababu wamewaandaa wasimamizi kwa kuwapa elimu ya usimamizi na uangalizi kuhakikisha hakutatokea udanganyifu.

Amewashauri wazazi kukaa na watoto wao vizuri na kuwa na ushirikianao na walimu wao kwa kipindi watakachokuwa wanasubiri matokeo na kuwatafutia sehemu ya kujifunza Kingereza kwa sababu watakapofaulu wataenda kufundishwa kwa lugha hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz