Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Imani potofu yatajwa kukithiri ugonjwa wa vikope Lindi

Vikope Lindi.png Imani potofu yatajwa kukithiri ugonjwa wa vikope Lindi

Tue, 30 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Imani potofu ya wananchi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, imetajwa kuwa sababu ya kukithiri kwa ugonjwa wa vikope kutokana baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo kuogopa matibabu ya macho wakidai kuwa watang’olewa macho.

Akizungumza jana Jumatatu Januari 29, 2024 kwenye kambi ya macho iliyofanyika katika zahanati ya Mpiruka wilayani humo, mkazi wa kijiji hicho Juma Bakari amesema kuwa jamii nyingi hazina uelewa wa ugonjwa wa vikope kutokana na imani potofu walionayo.

"Shida ni wananchi wanaoishi vijijini hawana uelewa wa kutosha wa ugonjwa wa vikope, ndio maana unakuta mtu anasumbuliwa na macho, lakini haendi hosptali na wanapokuja madaktari bingwa kuwatibia bure, hawajitokezi wakihofia kupoteza macho yao," amesema Juma.

Juma ameiomba Serikali na wadau wa maendeleo kutoa elimu ya kukabiliana na ugonjwa huo ili watu waachane na imani potofu.

Kwa upande wake Meneja wa mradi wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kutoka Shirika la Sightsavers Tanzania, Peter Kivumbi amesema mtu kupata upofu wa kudumu kutokana na kope kujikwaruza kila wakati kwenye kioo cha jicho na kutengeneza kovu.

"Wananchi wanatakiwa kuweka mazingira safi, kunawa na maji safi na salama mara kwa mara ili kuweza kujinga na ugonjwa wa vikope, kwani ugonjwa huu unaenezwa na inzi kutokana na uchafu," amesema Peter.

Naye Mratibu wa huduma za macho Mkoa wa Lindi, Dk Mwita Machage, amesema kwa utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya mwaka 2021-2022, Wilaya ya Ruangwa inaongoza kwa kuwa na wagonjwa 890, ikifuatiwa na Nachingwea yenye wagonjwa 885 na Liwale yenye wagonjwa 128.

Mwita amesema wanatarajia kuwafikia wagonjwa wote katika Wilaya za Nachingwea na Ruangwa hadi kufikia 2026 ili kuwapatia huduma ya usawazishaji.

"Shirika la Sightsavers linashirikiana na Serikali kuhakikisha ifikapo, 2026 wagonjwa waliofanyiwa utafiti wote wanapata matibabu na kuondokana ma upofu katika mkoa wetu wa Lindi," amesema Dk Mwita.

Tolibia Chinguile aliyepewa matibabu ameishukuru Serikali na shirika la Sightsavers kwa kuwasaidia kupata huduma hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live