"Ni Mungu tu ndiye ametutoa kwenye basi hili, maana mimi nilikuwa nimekaa kiti cha tatu kutoka kwa dereva," ameanza kwa kusimulia Shakira Rashidi na kuongeza…
"Sijui ningekuwaje, nampongeza dereva alijitahidi kumkwepa huyo dereva bodaboda lakini ilishindikana, kwenye kidole changu cha mwisho nimepata mchubuko kidogo," amesema Shakira huku akionyesha kidole chake.
Shakira ni mmoja wa mashuhuda wa ajali iliyotokea leo asubuhi Jumanne Septemba 12, 2023 katika makutano ya mataa ya Lumumba na Barabara Morogoro.
Ajali hiyo imehusisha basi la mwendokasi lillokuwa likitokea Kimara kwenda Kuvukoni na bodaboda ambaye bado hajafahamika jina lake na kuisababishia taharuki na usumbufu kwa baadhi ya magari yaliyokuwa yanatoka Barabara ya Morogoro kwenda mjini, Kariakoo na maeneo mengine.
Katika ajali hiyo abiria waliokuwa kwenye mwendokasi walifanikiwa kutoka salama isipokuwa mwanamke mmoja ambaye amepata mshtuko na huduma ya kwanza na abiria wenzake ambao walimtoa ndani ya basi la mwendokasi.
Dereva wa bodaboda ambaye anadaiwa alikuwa na abiria waliingia chini ya uvungu wa basi la mwendokasi na kunasa, huku pikipiki yake ikivunjika na juhudi za kuwaokoa ziliendelea.
Jeshi la Zimamoto na Ukoaji walifika eneo la tukio kwa ajili ya kuendelea na uokoaji wa dereva wa bodaboda.
Shuhuda mwingine, Clemence Benedict amesema alikuwa nyuma ya dereva bodaboda ambaye anadaiwa kuligonga basi.
"Mimi nilikuwa natokea Fire kwenda Lumumba, nilipofika kwenye mataa ya Morogoro na Lumumba nilisimama kulipisha basi la mwendokasi lililokuwa linatoka Fire kwenda Kuvukoni kwa sababu taa za kijani zilikuwa zimeruhusu basi hilo kupita," anasema Benedict na kuongeza.
"Nikiwa nimesimama ghafla bodaboda ilinipita na kwenda mbele na wakati akitaka kuvuka akakutana na basi la mwendokasi na basi likajaribu kumkwepa lakini haikuwezekana na badala yake akaligonga na kuingia uvunguni wa basi hili na kunasa," anasema.
Shuhuda mwingine aliyekuwa ndani ya basi hilo, Grace Singo amesema basi la mwendokasi lililokuwa nyumba yake na kwamba aliona abiria wakitoka kupitia madirishani, huku dereva akiwatangazia kuwa mbele kuna ajali imetokea hivyo abiria wawe watulivu.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kutokea kwa ajali hiyo polisi walifika eneo hilo na kuimarisha ulinzi.