Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ilichobaini TAKUKURU ukaguzi miradi ya Tsh. milioni 400 Mwanza

E0cd5f7adb9674e7c306daee933272dc.jpeg Ilichobaini TAKUKURU ukaguzi miradi ya Tsh. milioni 400 Mwanza

Mon, 13 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Maadili ya Umma na Utawala Bora mkoani hapa zimetembelea miradi ya zaidi ya Sh milioni 400 ili kujua maendeleo yake. Baadhi ya taasisi nyingine zilizoshiriki ukaguzi huo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Maadili na Utawala Bora nchini ni, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Miradi hiyo ni ile inayotekelezwa kwa fedha za kupambana na Covid-19 ambapo pia zimeelekezwa katika matumizi mengine ndani ya kata tatu wilayani Nyamagana mkoani hapa. Ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Sekondari Luchelele kwa gharama ya Sh milioni 80 ni sehemu ya miradi hiyo, ambapo wakaguzi walikuta ujenzi umefikia zaidi ya asilimia 80.

Mkuu wa Takukuru mkoa wa Mwanza, Frank Mkilanya alisema nia ya serikali ni kuona maadili ya utumishi wa umma kwa wanaosimamia miradi hiyo yanazingatiwa kwa kuepuka vishawishi vya rushwa ambavyo vimekua vikizorotesha maendeleo ya taifa. “Kiongozi wa umma usijihusishe na rushwa ili kulinda heshima na thamani ya ofisi za serikali,” alisema.

Wakaguzi hao pia walitembelea mradi wa ujenzi wa zahanati ya Bubale katika kata ya Buhongwa inayopanuliwa ili kuwa na hadhi ya kituo cha afya. Upanuzi huo unahusisha unahusisha ujenzi wa wodi ya wazazi, maabara, sehemu ya kuchomea taka na shimo la maji taka kwa gharama ya Sh milioni 250 na ujenzi uko hatua za mwisho.

Mradi mwingine uliotembelewa ni ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Sekondari Pamba kwa gharama ya Sh milioni 124 ambapo Sh milioni 80 zimeshatolewa na ujenzi ulikutwa upo asilimia 30. Kaimu Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Umma na Utawala Bora Kanda ya Ziwa, Abigail Majige aliwasistiza watumishi wote wa umma kuzingatia miiko na maadili ili kujenga taifa lenye usawa na haki.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live