Wakazi wa vijiji mbalimbali katika Kata ya Maboga Jimbo la Kalenga wilayani Iringa wamesema hofu imezidi kutanda kutokana na ng’ombe wao kuzidi kuvamiwa na kuuawa hali ambayo inawafanya kushindwa kuendelea na majukumu yao ya kila siku wakihofia usalama wao.
Wananchi hao wameeleza kwamba hali inayoendelea inawafanya kubadilisha mfumo wa maisha yao kijijini hapo hasa katika shughuli zao za kila siku kama kilimo na nyinginezo.
Wamesema mpaka leo ni siku nne zimetimia tangu simba hao wafike katika maeneo yao kuvamia na kuua ng’ombe kwa kuhama hama kutoka kijiji kimoja mpaka vijiji jirani.
Wanamaboga wamesema wanatumia njia ya kutembea kwa makundi makundi mda wa mchana pamoja na kuwahi kurudi majumbani kabla ya saa 12 jioni, ili kujikinga na kuweza kuwakwepa simba hao hatari wanaowaumiza vichwa wananchi hao.
‘’Usalama bado kabisa kwa maana mtu kama unajua unaishi na simba sehemu moja ni lazima tu utakuwa na wasiwasi wa hali ya juu, tunazidi tu kuomba hao wanyama wapatikane na amani itawale,’’amesema Mhise mmoja wa wanakijiji cha Magumga.
Kwa upande wake Mussa Kisinini mkazi wa Kijiji hicho ameeleza kuwa kutokana na hali inayoendelea katika eneo hilo bado Askari wa wanyama pori wanafanya njia mbalimbali kuwasaka wanyama hao hatari.
Lakini pia baadhi ya wananchi wameeleza kuwa wanapata shida kujisaidia nyakati za usiku huku njia wanazotumia ni kuamshana nyumba nzima ili kwenda kwa pamoja mpaka mazingira ya choo huku wakitumia tochi kwani wanaamini simba hao wanaogopa mwanga.
Hata hivyo baadhi yao wameeleza kuwa wanaingia na ndoo ndani kwa ajili ya kujisaidia nyakati za usiku, kitu kinachowanyima uhuru kwani familia nzima inakuwa ikitegemea ubunifu huo.
Akizungumza leo Juni 17 Kamanda wa Hifadhi ya Taifa Ruaha Godwell Ole Meing'ataki amesema hana uhakika juu ya simba hao kutokea Ruaha na kuvamia vijiji vya jirani, lakini kwa kushirikiana na Askari wa Wanyama pori vikosi vinaendelea kupelekwa ili kutatua changamoto hiyo.
Ole Meing'ataki ameeleza kwamba vijiji vilivyovamiwa na simba hao ni maeneo jirani na hifadhi ya Ruaha hivyo kama simba hao wameweza kutembea na kufika maeneo ya wananchi hivyo ni dhahiri simba hao wamekumbwa na njaa ambayo imewasababisha kutafuta chakula kwa njia yotote.
Ameendelea kufafanua kwamba jitihada za kuwatafuta simba hao bado zinafanyika japokuwa kumekuwa na shida ya kuweza kuwakamata isipokuwa askari wa doria wamethibitisha kumuona simba na watoto kadhaa.
Ole Meing'ataki amesema kuna vifaa mbalimbali ambavyo vimeandaliwa ili kuweza kuwakamata simba hao na kuwarudisha hidfadhini hivyo amewaomba wananchi wawe wavumilivu na kuwa makini huku Askari wa wanyamapori wakiendelea na kazi yao ya kuwatafuta simba hao.
''Hatutaki kumpoteza mwanakijiji hata mmoja hivyo tunafanya kila namna kuwapata simba hao na kuwarudisha hifadhini,"amesema Ole Meing'ataki .
Diwani wa Kata ya Maboga Wilayani Iringa Venserus Muyinga amethibisha kuwepo kwa simba hao wakiwa bado wanaendelea kuvamia vijiji mbalimbali vya kata hiyo.
Muyinga amesema Askari wa wanyamapori wanaendeleza juhudi za kuwatafuta huku kikosi kingine kikitumwa leo ili kuungana na vile viwili vya mwanzo kwa ajili ya kuleta nguvu.
Diwani amewaomba wanakijiji wanaokumbwa na adha hiyo kuwa na usikivu kwa yale wanayoelekezwa na wataalamu wa wanyamapori, huku akiwakumbusha kurudi nyumbani mapema, kupunguza kunywa pombe ili kuepusha madhara zaidi.
“Simba ni hatari jamani tujaribu kupunguza pombe kidogo, itakuwa ajabu mtu umekunywa unakutana na simba unajikuta unaomba samahani kwa mnyama huyo kitu ambacho ni cha kushangaza”alisema Muyinga.