Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hukumu ya maofisa usalama Posta Desemba 28

HUKUMU Hukumu ya maofisa usalama Posta Desemba 28

Tue, 5 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Desemba 28, mwaka huu kutoa hukumu katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya kwa njia ya posta, inayowakabili maofisa usalama watatu wa shirika hilo.

Maofisa hao ni George Mwamgabe, Sima Ngaiza na Abdulrahman Msimu, wanadaiwa kusafirisha dawa hizo kwa kutumia Shirika la Posta.

Uamuzi huo umetolewa leo Desemba 5, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate, baada ya washtakiwa hao kufunga utetezi wao.

Washtakiwa waliwasilisha mashahidi wanne na vielelezo kwa ajili ya kujitetea, wakati upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi wanane kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.

Washtakiwa wanadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi gramu 124.55 na heroine gramu 1.55, kosa walilodaiwa kulitenda Agosti, 2018 katika ofisi za Posta, Ilala jijini Dar es Salaam.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutumia Shirika la Posta, kusafirisha dawa hizo zikiwa katika vifurushi kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro, wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Hemed Halfan akisaidiana na Eva Kassa walidai kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya washtakiwa kuendelea kujitetea baada ya kukutwa na kesi ya kujibu.

Katika utetezi wao, washtakiwa hao walidai kuwa tuhuma zinawakabili si za kweli na wanaiomba Mahakama iwaachie huru.

Washtakiwa baada ya kumaliza kujitetea, walifunga utetezi wao na hakimu Kabate alipanga tarehe ya kutoa hukumu.

“Washtakiwa mtaendelea kuwa nje kwa dhamana na Mahakama hii itatoa hukumu Desemba 28, mwaka huu,” amesema Hakimu Kabate na kisha kuahirisha kesi hiyo.

Agosti mosi, 2023, Mwamgabe na wenzake walikutwa na kesi ya kujibu, baada ya mahakama kupitia ushahidi wa mashahidi wanane na vielelezo tisa vilivyotolewa na upande wa mashtaka.

Baada ya kukutwa na kesi ya kujibu, washtakiwa waliieleza mahakama hiyo kuwa watajitetea kwa kiapo na watakuwa na mashahidi pamoja na vielelezo kadhaa.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kusafirisha dawa hizo Agosti, 2018 katika ofisi za Posta, Ilala jijini Dar es Salaam, kinyume cha Sheria.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live