Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hukumu kesi ya DC Chemba kutolewa Septemba 18

75595 Pic+chemba

Fri, 13 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo Ukonga wilayani Ilala imesema Septemba 18, 2019  itatoa hukumu kesi ya madai ya talaka iliyofunguliwa na mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga dhidi ya mkewe, Medilina Mbuwuli.

Hukumu hiyo ilipaswa kutolewa leo Ijumaa  Septemba 13,2019   lakini Hakimu Christina Luguru ameiahirisha hadi tarehe hiyo kwa maelezo kuwa hajamaliza kuiandaa.

Wakati kesi hiyo ikiahirishwa, aliyekuwepo mahakamani hapo ni Medilina pekee huku ndugu wa mkuu huyo wa wilaya wakieleza kuwa alikuwa njiani.

Baada ya kusikiliza maelezo ya pande hizo mbili, hakimu Luguru alitaja tarehe hiyo.

Odunga na Medilina  wanadaiwa kufunga ndoa ya kanisani mwaka 2000 na kupata cheti cha ndoa  A no 00140917.

Sehemu ya ushahidi wa wawili hao

Pia Soma

Advertisement
Agosti 15, 2019 Odunga alidai kuwa huwa anatoa matunzo ya mtoto wao wa kike ambaye kwa sasa anasoma kidato cha sita aliyezaa na Medelina.

Alieleza hayo alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi ya madai ya talaka namba 181 ya mwaka huu aliyoifungua katika Mahakama hiyo.

Odunga, akitoa ushahidi huo mbele ya Hakimu  Luguru alisema anaomba talaka kwa sababu ametengana na mkewe huyo tangu mwaka 2003 na kwamba katika maisha yao ya ndoa, walikuwa wakigombana mara kwa mara kiasi cha kutengana na kipindi chote hicho alikuwa hana kazi. Alidai kuwa ilipofika mwaka 2002 alipata kazi akapanga nyumba eneo la Makuburi akamfuata mkewe wakasuluhishwa na wakarudiana kuishi pamoja.

“Baada ya kusuluhishwa tuliishi hadi mwaka 2003 pamoja, lakini hatukuwa na maelewano, siku moja nilipokuwa kazini mke wangu aliamua kuhama nyumba bila kunitaarifu.”

Alidai kuwa baada ya mama huyo kuondoka, alikaa na familia yake wakashauriana kuwa amtafute kwa ajili ya kumtunza mtoto na wakati huo alikuwa anasoma shule ya awali.

Alidai kuwa aliwahi kwenda katika shule ya awali aliyokuwa akisoma mtoto wao na kukuta ameandikishwa kuwa ana mzazi mmoja na kwamba baba yake alishakufa hivyo alikataliwa.

“Nilirudi kwa familia za pande zote mbili tukafanya kikao na mke wangu aligoma kuishi na mimi akidai niendelee kumtunza mtoto, kikao kiliamua nimpatie talaka, hatua ambayo sikuitekeleza hadi sasa ninapoiomba hapa mahakamani,” alieleza Odunga.

“Ila nimekuwa nikipeleka matunzo ya mtoto nyumbani kwake, lakini kuna siku nilishambuliwa, nikazuiliwa kwenda.”

Alidai kuwa amekuwa akimlea mtoto wake kwa tabu kwa sababu mdaiwa hataki aende nyumbani kwake, lakini ameendelea kutoa huduma kama ada kwa kumpatia mama yake. Alidai pia kwamba mtoto huyo alifaulu lakini mama yake alimpeleka shule binafsi, “hivyo nilikuwa nikitoa huduma kulingana na uwezo wangu.”

Kutokana na maelezo hayo, aliomba mahakama iivunje ndo hiyo kwa kuwa ilishindikana kusuluhishwa ngazi ya familia ambayo ilimpatia baraka ya kutoa talaka.

Baada ya Odunga kutoa ushahidi huo, Medelina alimuuliza kama alishawahi kwenda kanisani kabla ya kufika mahakamani na alijibu kuwa alienda mwaka 2001 na 2003.

Medelina alimuuliza tena Odunga kama alikuwa akitoa ada ya shule ya mtoto tangu mwanzo, anaweza kukumbuka jina la shule aliyokuwa akisoma mtoto wao na kujibu kuwa hakumbuki ila anajua mahali ilipo na sasa hajui anasoma wapi.

Alimuuliza tena kama anaweza kuithibitishia mahakama hata kwa risiti za ada na Odunga alidai kuwa alikuwa akimpa fedha taslimu.

Shahidi wa Odunga, Godol Odunga (61) maarufu Ogonda alidai kuwa mdai na mdaiwa walifunga ndoa ya Kikristo lakini hakumbuki ilikuwa lini na mwaka 2003 walitengana na kila mmoja aliishi peke yake.

Alidai kuwa kati ya mwaka 2012 na 2013 kikao cha ukoo kilikaa na Odunga alidai kuwa anataka kuoa mke mwingine na akaagizwa kama anataka hiyo atoe talaka kwanza.

Baada ya kutoa ushahidi huo, Medelina alimuuliza wewe ni mtumishi wa Mungu ulishawahi kuona ndoa ya kanisani inavunjwa mahakamani? Shahidi huyo akajibu, “mimi nasema ninachojua.”

Kesi nyingine ya madai ya talaka iliyofunguliwa na Odunga mahakamani hapo dhidi ya ndoa aliyoifunga serikalini na Ruth Osoro nayo ilitolewa uamuzi kwa mahakama kusema kuwa haiitambui ndoa hiyo kwa kuwa ni batili huku ikimtaka mkuu huyo wa wilaya kulipa gharama za matunzo ya mwanaye kila mwezi

SOMA ZAIDI

> Mke mwingine agomea talaka ya DC kortini

> Mahakama yatupa ombi la DC Chemba kutaliki, yamtaka kutoa Sh250,000 kila mwezi za mtoto

> Mkuu wa wilaya ya Chemba afungua kesi, ataka kuwataliki wake zake wawili

> Kesi ya DC Chemba kumtaliki mkewe yapigwa kalenda hadi Agosti 5

Chanzo: mwananchi.co.tz