Arusha. Hoteli maarufu za kitalii mkoani hapa za Impalla na Ngurdoto Mountain Lodge zimetangazwa kuuzwa na benki ya Exim (T) Limited.
Hoteli hizo ambazo zinamilikiwa na wafanyabiashara kadhaa nchini, mkurugenzi wake mkuu, Melau Mrema alifariki dunia mwaka juzi zinauzwa na kampuni ya uwakili ya Locus Attorney ya jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa tangazo la kuuzwa kwa hoteli hizo, mnunuzi anatakiwa kutuma zabuni kwa kampuni hiyo kupitia wakili Dk Onesmo Kyauke kabla ya Aprili 15.
Hata hivyo, mmoja wa wakurugenzi wa benki hiyo ambaye hakutaka kutatajwa alisema hana taarifa za kudaiwa na beki hiyo. “Tumeshangazwa na hili tangazo Exim hawatudai tunadaiwa na NBC ambao ndiyo wana hati zetu na leo nimewauliza kuhusu deni hili nao wameshangaa,” alisema mkurugenzi huyo.
Alisema wanafuatilia kujua chanzo cha tangazo hilo ambalo pia linataja viwanja viwili vya hoteli ya Impalla.
Hata hivyo,Dk Kyauke jana alipotakiwa kuelezea juu ya tangazo hilo alijibu kwa ujumbe wa simu kuwa yupo kortini.
Akizungumzia tangazo hilo, katibu wa mtandao chama cha wamiliki wa kampuni za Utalii Tanzania (Tato), Sirili Ako alisema wameliona lakini wanachohitaji watalii wapate huduma bora.
“Nimeona tangazo Tato hatuhusiki kufuatilia umiliki wa hoteli tunataka watalii wapate huduma bora,” alisema.
Hoteli za Impalla na Ngurdoto ni maarufu nchini kwani zimekuwa zikipokea watalii na mikutano mikubwa ya kimataifa. Hata hivyo, siku za karibuni mikutano imepungua huku ile ya Serikali ikifanyika katika kumbi za Serikali.
Ngurdoto Mountain Lodge ilipata umaarufu wakati wa Serikali ya awamu ya tatu na nne kwa kupokea mikutano mingi ikiwamo mikutano ya semina elekezi.