Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hoteli 100 Dar matatani kwa kuchimba visima bila kibali

Tue, 20 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Bodi ya Maji ya Wami/Ruvu inakusudia kuzifikisha mahakamani hoteli na kampuni ambazo zimechimba visima bila kibali na hazilipi ada ya kila mwaka, kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji ya mwaka 2009.

Hata hivyo, baadhi ya wadaiwa wamesema hawakuwa na taarifa za kutakiwa kulipa ada hizo na wengine wakiahidi kulipa tozo hizo kwa mujibu wa sheria hiyo.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa wa Maji katika bodi hiyo, Simon Ngonyani alisema hoteli 100 zimebainika kutolipa ada hiyo jijini hapa, zikiwemo kampuni 25 za mafuta na makampuni mengine 22.

“Tulipotangaza kampuni zinazochimba visima zijisalimishe, zimejitokeza kampuni 98 pekee. Kamati tuliyoiunda inaendelea na kazi ya kufuatilia wote ambao hawajafanya hivyo na kwa kuanzia tutawafikisha hawa mahakamani keshokutwa (Jumatano),” alisema.

Ngonyani alibainisha kwamba Sheria ya Usimamizi wa Maji ya mwaka 2009 inamtaka kila mtu au taasisi inayochimba kisima kuwa na kibali na kulipa ada ya kila mwaka kulingana na kiasi cha maji kinachovunwa kwenye kisima chake.

Alisema wanatarajia kukusanya zaidi ya Sh200 milioni kama malipo ya mwaka huu pekee endapo hoteli na kampuni hizo zitalipa. Aliongeza kuwa zipo kampuni zenye malimbikizo ya ada kwa miaka iliyopita na kwamba wanatakiwa kuzilipa.

“Tunawadai pia Dawasa (Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam) lakini wao wameanza kulipa, tulikubaliana kwamba watakuwa wanatulipa kwa awamu, tayari wameanza kufanya hivyo, wametulipa zaidi ya Sh400 milioni.”

“Sheria hii haibagui, hata taasisi za Serikali zenye visima zitatakiwa kulipa ada stahiki. Wenzetu Dawasa wameanza kutulipa, kamati yetu inaendelea na kazi kubaini wadaiwa wengine,” alisema Ngonyani.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, meneja wa Hoteli ya Kebby’s ambayo ni miongoni mwa wadaiwa, Joseph Maina alisema hawajafanya malipo kwa sababu mtu mwenye nyaraka za malipo yaliyopita hayupo.

“Tutawasiliana nao tuone tunafanyaje. Kilichotuchelewesha ni mtu mwenye document za malipo hayupo, kwa hiyo tunashindwa tufanye malipo kuanzia lini,” alisema meneja huyo na kuongeza kuwa hakuwa na taarifa za kutakiwa kujisalimisha mapema.

Meneja wa hoteli ya Lamada, Martin Wamanya alisema hakuwa na taarifa za kudaiwa na Bodi ya Maji ya Bonde la Wami/Ruvu. “Labda niulize kwa department (idara) nyingine, wanaweza kuwa wana taarifa lakini mimi hazijanifikia.”



Chanzo: mwananchi.co.tz