Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali ya Temeke kuanza ujenzi wa ghorofa

Mollel Temeke Hosp.png Hospitali ya Temeke kuanza ujenzi wa ghorofa

Tue, 21 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali kupitia Wizara ya Afya tayari imetenga Sh7.9 bilioni kuanza ujenzi wa upanuzi wa Hospitali ya Rufaa ya Temeke kwa kujenga majengo ya kwenda juu (ghorofa), ili kupambana na changamoto ya ufinyu wa eneo.

Hatua hiyo inakuja baada ya gazeti hili Agosti 22 kuchapisha habari ya uchunguzi kuhusu kukosekana kwa mipango miji katika ujenzi wa hospitali za rufaa mkoani Dar es Salaam, na namna kutakavyoigharimu Serikali kwa kulazimika kubomoa baadhi ya majengo.

Ukosefu wa mipango hiyo na ufinyu wa maeneo umekua kikwazo katika uendelezaji na upanuzi wa huduma kulingana na ongezeko la idadi ya watu, na hadhi ya hospitali husika ambapo awali ilianza kutoa huduma kama zahanati.

Akizungumza leo Jumatatu, Novemba 20, 2023 Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel akiwa katika ziara ya kutembelea Hospitali za rufaa Temeke na Mwananyamala kwa lengo la kufuatilia na kusimamia ubora wa huduma amesema tayari hospitali hiyo ilishapatiwa Sh4.9 bilioni na wametengewa bajeti ya Sh3 bilioni kwa mwaka huu wa fedha.

Amesema hospitali hiyo inahitaji upanuzi na kuna majengo ni ya kubomoa kisha wajenge kwenda juu akitokea mfano Saifee za Serian ya Arusha zenye jengo moja la vitanda 600 kwa kuwa imejengwa kwenda juu.

Amewataka wahakikishe kunakuwa na miundombinu rafiki kwa ajili ya wagonjwa zikiwemo lifti.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda amemuomba Dk Mollel kuangalia namna wizara hiyo itakavyotenga fedha kwa ajili ya upanuzi wa hospitali hiyo na kujenga Hospital ya Wilaya ya Temeke.

"Wizara ituangalie, Temeke ilianza kama zahanati na si kituo cha afya kwa sasa ni hospital ya rufaa eneo hili halijawahi kuongezeka hata hatua moja. Mrundikano ni mkubwa kwani huduma nyingi sasa zinatolewa hapa.

"Ututazame kwenye bajeti zako tujenge maghorofa, hatuwezi kwenda kulia wala kushoto tunahitaji kwenda juu, tunaweza kwa kwenda juu lifti zikawekwa na kwa maana eneo la Chamazi kuna Ekari 30, mmetuletea milioni 600 tunazo lakini hatuna pa kujenga, kama Muhimbili watakubali kutupatia eneo tupo tayari kujenga hata kesho,”amesema Mapunda.

Naye Mbunge wa jimbo la Temeke, Dorothy Kilave amesema Temeke inahudumia watu wengi hivyo akaomba majengo yaongezeke na kama kuna uwezekano kuongezwe hospitali ya wilaya.

Awali akizungumzia ubora wa huduma Dk Mollel amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameshafanya jukumu la kuboresha miundombinu , kwa hiyo kazi iliyobaki ni kwa watoa huduma.

"Nimetembelea na kuona vifaa vilivyonunuliwa, suala la ubora wa huduma naagiza kila mkoa kuna timu za usimamizi wa huduma lazima zifike kule chini na kuwajengea uwezo watumishi, kutatua changamoto zilizopo na kuzizuia mapema.

"Ngazi ya Wilaya yupo DMO na timu yake, yanapotokea matatizo kwenye timu za afya inabidi viongozi wajitafakari walikuwa wapi mpaka tatizo likatokea.

Amesema jambo lisipoenda vizuri katika eneo la huduma za afya kuna mtu anapata ulemavu na kuna mtu anapoteza maisha, vifo vya kina mama wengi na watoto wachanga visitokane na uzembe.

"Mtanzania yeyote akipata shida viongozi wote wa eneo husika ni watuhumiwa pamoja na aliyefanya kosa, viongozi wengi wanauza sura tu hawafanyi kazi yao wanazunguka zunguka tu," amesema Dk Mollel na kuagiza kwamba hilo ni agizo la nchi nzima.

Kwa upande wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Temeke, Dk Joseph Kimario amesema Serikali imenunua vifaa vya bei ghali vyenye teknolojia na ubora wa huduma ikiwemo CT scan na mashine ya kisasa ya X Ray.

"CT Scan imenunuliwa bilioni 2 na ina uwezo wa kutibu watu 150 kwa mwezi,”amemalizia kusema Dk Kimario.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live