Hospitali mpya ya Rufani mkoani Shinyanga iliyopo Mwawaza Manispaa ya Shinyanga haina jengo la kuhifadhia Maiti, pamoja na kukabiliwa na upungufu mkubwa wa madaktari bingwa.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Yudas Ndugile amebainisha hayo jana kwenye ziara ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu mkoani humo.
Alisema hospitali hiyo ilianza kutoa huduma za matibabu Novemba mwaka jana na kwamba serikali ilitoa Sh.bilioni tisa ili kuikamilisha, bilioni tano zilitumika ujenzi wa majengo na bilioni nne ununuzi wa vifaa tiba, lakini hadi sasa haina jengo la kuhifadhia maiti.
“Hospitali hii ina hudumia wagonjwa 150 hadi 200 kwa siku na tunalaza wagonjwa 60 hadi 80 kwa siku moja ya changamoto ambayo tunayo kwenye hospitali yetu hatuna jengo la kuhifadhia maiti,” alisema Dk. Ndugile.