Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali ya Bombo yaingia kwenye mvutano na ndugu wa mgonjwa

Hospitali Ya Bombo Hospitali ya Bombo yaingia kwenye mvutano na ndugu wa mgonjwa

Tue, 10 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Tanga (Bombo) imeingia katika mgogoro na familia ya Rahma Matola, wakazi wa Mtaa wa Mtakuja, Kata ya Makorora mkoani Tanga kutokana na kile walichodai ndugu yao kutopatiwa matibabu stahiki.

Vilevile, kutokana na hali hiyo wamedai waliamua kumhamishia ndugu yao Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako hadi sasa kuna deni la Sh. milioni nne ambalo wanaitaka Hospitali ya Bombo kulilipa.

Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, mume wa Rahma, Akida Akida alidai mke wake alilazwa Hospitali ya Bombo Novemba 11, mwaka jana, kwa ajili ya matibabu lakini baadaye ilibidi afanyiwe upasuaji kwenye tumbo.

Alidai kuwa mkewe alikuwa mjamzito wa miezi saba na baada ya kupimwa, daktari wa Bombo alishauri afanyiwe upasuaji ambao ulifanyika Novemba 15, mwaka jana.

"Mke wangu huwa anajifungua kwa upasuaji, baada ya upasuaji, walibaini kiumbe kilishafariki dunia, wakamfanyia matibabu wakamshona lakini baada ya siku mbili, hali ilibadilika akavimba mwili mzima. Niliwahoji madaktari walidai ni kawaida kwa mgonjwa wa aina hiyo," alidai.

Akida alidai kuwa hali ya mkewe ilizidi kuwa mbaya kutokana na uvimbe kuongezeka huku akilalamika kuwa na maumivu makali.

"Baada ya muda tulijulishwa kuwa itabidi mgonjwa afanyiwe upasuaji mwingine na Novemba 21 mwaka jana alipasuliwa kwa mara ya pili lakini hali ilizidi kuwa mbaya na safari hii hadi ulimi ulivimba," alidai.

Aliendelea kuwasilisha madai yake kwa ilipotimu Novemba 27, mwaka jana, aliwaomba madaktari wampe mgonjwa rufani ili ampeleke Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.

"Nilikubaliwa kumchukua mgonjwa ila nikatakiwa kuchangia nauli ya gari la wagonjwa Sh. 350,000 na nitapewa muuguzi mmoja, lakini baadaye walisema gari ni bovu na muuguzi ana mtoto mchanga, niliwaambia niko tayari kukodi gari binafsi ila ninaomba muuguzi na gesi ya mgonjwa (Oksijeni) imsaidie akiwa njiani, lakini sikupewa vyote," alidai.

Akida pia alidai kuwa waliomba kibali cha kumwondoa mgonjwa hospitalini huko, nacho walinyimwa na walipewa kitabu cha kutia saini kuwa waliamua kumchukua mgonjwa kwa hiari yao wenyewe bila ridhaa ya daktari.

Kwa mujibu wa Akida, walimchukua mgonjwa wakampeleka Muhimbili ambako walifika Novemba 28 mwaka jana, lakini hawakupokewa kwa kuwa hawakuwa na kibali kutoka Hospitali ya Bombo.

"Mke wangu alikaa eneo la mapokezi kwa saa nane lakini baada ya majadiliano ya kina kati ya familia na madaktari wa Muhimbili, walimpokea na kumpatia matibabu," alidai.

Akida alidai kuwa kwa gharama za matibabu hadi juzi (Jumamosi) zimefikia Sh. milioni nne na kwamba kwa kuwa anaona kuna uzembe uliofanyika Bombo, Hospitali hiyo ya Rufani ya Mkoa wa Tanga inapaswa kulipa gharama hizo za matibabu Muhimbili.

Alipotafutwa na Nipashe kuzungumzia suala hilo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Tanga, Naima Zakaria alikiri hospitali hiyo kumpokea mgonjwa huyo.

Pia alikiri mgonjwa huyo kufanyiwa upasuaji, lakini mara moja, kwa tatizo la uzazi, akikana madai ya Akida ya kufanyika upasuaji wa pili kwa mgonjwa huyo. Kiongozi huyo wa hospitali alifafanua kuwa ugumu wa kutoa rufani kwa mgonjwa huyo ulitokana na hisia kwamba ndugu zake walitaka kumpeleka mgonjwa wao kwenye tiba mbadala.

Alisema kuwa kutokana na hali aliyokuwa nayo mgonjwa huyo, daktari alishauri afanyiwe Dialysis (kusafisha damu) na siyo kupelekwa kwenye tiba mbadala lakini ndugu waliamua kumchukua mgonjwa bila idhini ya daktari.

Kwa mujibu wa daktari huyo, mgonjwa alifanyiwa upasuaji mara moja tu kutokana na kuwa na makovu mawili kwenye mfumo wa uzazi na pia alikuwa ameshaanza kuvuja damu sehemu za siri.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live