Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hoja ya muda, lugha ya Kiingereza yawakimbiza wadau mkutanoni

70024 Pic+latra

Mon, 5 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wamiliki wa vyombo vya usafiri wa ardhini pamoja na madereva Tanzania wamesusia mkutano wa kupokea maoni ya wadau katika rasimu ya kanuni za sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kutokana na kile walichoeleza lugha iliyotumika katika rasimu hiyo na muda waliopewa kabla ya mkutano huo.

Mkutano huo umefanyika leo Jumatatu Agosti 5, 2019, Viongozi wa Serikali husani Wizara ya uchukuzi pamoja na wadau wengine katika sekta hiyo waliohudhuria huku kila upande ukiwa na wanasheria wake.

"Kabrasha tulilopewa tulitolee maoni lina kurasa 115 na tulipewa siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita leo hii wanataka tutoe maoni wakati hatujapata muda wa kupitisha rasmu yenyewe hapa tumewaomba walau watupe wiki mbili tuipitie ili tuweze kutoa maoni wanataka tufanye leo sasa sijui hiyo haraka ni ya nini," amesema Katibu mkuu wa chama cha wamiliki wa mabasi (Taboa) Enea Mrutu.

Mrutu amesema mbali na kupata rasmi hiyo kwa kuchelewa bado ilikuwa katika lugha moja ya Kiingereza tu wakati wadau wanaelewa lugha tofauti hivyo walitaka rasmi hiyo iwe na tafsiri ya Kiswahili ili ieleweke kwa watu wote.

"Tunahitaji tukae na madereva tushauriane watupe maoni yao sisi viongozi kila mtu ana maoni yake, madereva wapo wengi wapo ambao wanaweza kusoma hiyo rasmi wakaelewa maana wapo hadi wenye digrii zao waliokosa kazini lakini bado hata hao wanahitaji muda ili kutoa maoni thabiti," amesema Mrutu.

Makamu mwenyekiti wa Chama cha wamiliki wa Maroli (Tatoa) Elias Lukumy  amesema mkutano ulikuwa na lengo zuri lakini muda uliotolewa ulikuwa hautoshi kusoma kwa kina kabrasha lile ambalo ni muhimu kwa mustakabali wa sekta ya usafiri na uchukuzi Tanzania.

Pia Soma

 

"Tunahitaji kupata muda kupitia nyaraka, kuna kanuni zina mkanganyiko kuna changamoto katika kanuni za udereva, wamiliki na makosa yanayosimamiwa na kutozwa faini na Latra na jeshi la polisi," amesema Lukumy.

Hata hivyo, baada ya wadau hao kutoa hoja hizo Mkurugenzi wa uchukuzi wa Wizara ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano, Aron Kisaka amesema wamepokea maoni hayo ya wadau na yatafanyiwa kazi.

"Tumewaeleza kuwa hapa wasikilize tu ili kupata uelewa na maoni watatoa baada ya siku 14 kama walivyotaka na hilo la lugha ndani ya siku saba tutawapa nakala ya Kiswahili lakini wamekataa," amesema Kisaka.

Chanzo: mwananchi.co.tz