Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hofu yatanda wanawake wanne kuuawa, kunyofolewa viungo

10088 Wanne+pic TanzaniaWeb

Sat, 4 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Misungwi. Wakati polisi mkoani Mwanza inawashikilia watu watatu wakihusishwa na tukio la mauaji ya wanawake wanne, hofu imetanda katika vijiji vya Misasi, Isakamawe na Mabuki wilayani Misungwi.

Miili ya wanawake hao imepatikana maeneo tofauti ikiwa haina baadhi ya viungo kama ulimi, matiti na sehemu za siri.

Kufuatia hali hiyo hofu imetanda miongoni mwa wakazi wa vijiji hivyo kutokana na miili hiyo kukatwa viungo hivyo na pia kukutwa na alama za kunyongwa kabla ya kufanyiwa unyama huo.

Akizungumza na Mwananchi, John Makoye mkazi wa Isakamawe aliyeshuhudia marehemu hao alivitaja viungo hivyo kuwa miongoni mwa vile vilinyofolewa katika miili ya marehemu.

Jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi aliwataja waliouawa kuwa ni Angelina Lumala (45), mkazi wa kijiji cha Isakamawe na Ngole (43) mkazi wa Kitongoji cha Bujingwa, Kijiji cha Mabuki. Wengine ni Kundi Laurent (35) na Mariam Manila (30) wote wakazi wa kijiji cha Misasi.

Alisema tayari polisi inawashikilia kwa mahojiano watu watatu ambao hakuwa tayari kuwataja majina waliokutwa kwenye mapori ambako miili hiyo ilikutwa.

Akizungumza na familia za marehemu baada ya kuzitembelea, Kamanda Msangi aliwaomba wananchi wenye taarifa zitakazosaidia kuwanasa wauaji kujitokeza kusaidiana na polisi.

Alisema, “tutawasaka na kuwatia mbaroni wote waliohusika na matukio haya,” alisema.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Marco Peter aliwataka akinamama wanaokwenda porini kukata kuni kuchukua hatua kwa kutembea wakiwa katika makundi ikiwezekana waongozane na waume zao.

“Viongozi wa vitongoji na vijiji nao wanapaswa kuimarisha vikundi vya ulinzi wa jadi maarufu kama Sungusungu katika maeneo yao kwa ajili ya ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao,” alisema Peter.

Chanzo: mwananchi.co.tz