Wakazi wa Kitongoji cha Mkoga, Kata ya Tambani Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani wameingiwa na hofu baada ya kudai wamekula ubwabwa wa sherehe ya harusi na kuugua matumbo usiku wa kuamkia jana Jumatatu.
Taarifa zilizosambaa katika kitongoji hicho kuanzia leo Jumatatu Januari 16, 2023 asubuhi, baada ya baadhi ya watu kuugua matumbo na kulazimika kumeza dawa za flagyl ili kupunguza maumivu ya tumbo.
Mama mmoja ambaye hakupenda kutaja jina lake, amesema tangu amekula chakula cha sherehe muda mfupi baada ya sherehe hiyo ya harusi kuisha saa 9 alasiri jana, ilipofika jioni tumbo lilianza kumuuma.
“Yaani hapa mtaani mimi na watoto wangu, wote tunaumwa matumbo na majirani zangu wengine waliohudhuria sherehe hiyo wote wanaumwa matumbo,” amesema.
Mwathirika mwingine aliyejitambulisha kwa jina, Ramadhani Mdoe amesema tumbo lilimuuma mara moja tu hata hivyo anapata hofu kwa nini watu wengi waumwe matumbo.
Awali, zilienea taarifa miongoni mwa wananchi hao kuwa huenda wamekula chakula kilichodhaniwa kuwa na sumu.
Mwenyeketi wa Kitongoji cha Mkoga, Amani Kibwana alipotafutwa kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, aliomba kuwasiliana na mjumbe wa eneo hilo ili kujua zaidi nini kilichotokea.
Hata hivyo, muda mfupi baadaye mwenyekiti huyo alipiga simu kwa mwandishi na kueleza kuwa, baada ya kuwasiliana na wahusika wa familia, aliwataka kufika ofisi za kijiji ili kutoa maelezo.
Hata hivyo mhusika huyo alikuwa mbali lakini alifanikiwa kutoa ufafananuzi kwa njia ya simu kwamba katika sherehe hiyo, kulikuwa na nyama ambazo zilinunuliwa siku mbili kabla ya harusi.
“Kulikuwa na nyama ambazo zilinunuliwa siku mbili kabla na uhifadhi wake haukuwa mzuri kwa kuwa haikukaushwa. Hivyo wapo waliokula pilau na maharage pekee, wapo waliokula pilau na nyama hao ndio wengi na ndio waliodhurika,” amefafanua Kibwana.
Amesema hata hivyo hakuna mtu yeyote aliyeripotiwa kulazwa hospitali kutokana na tukio hilo.