Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hofu yatanda mvua ikinyesha Dar, Zanzibar

Mafuriko Hali Ilivyo.png Hofu yatanda mvua ikinyesha Dar, Zanzibar

Mon, 13 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakazi wa Dar es Salaam wanaotumia Barabara ya Morogoro jana walikumbana na adha kutokana na kufurika kwa maji yaliyosababishwa na mvua eneo la Jangwani, hivyo kushindwa kupitika kwa muda.

Mafuriko katika daraja hilo na maeneo mbalimbali ya jiji hilo pamoja na visiwani Zanzibar, yalitokana na mvua zinazoendelea kunyesha, ambazo awali Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilizitangaza.

Kwa mujibu wa taarifa ya TMA, mvua hizo zilitabiriwa kunyesha jana katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Lindi na Morogoro, huku ikiwataka wakazi wa maeneo hayo wachukue tahadhari.

Lakini, kufurika maji kwa daraja la Jangwani na maeneo ya mabondeni si jambo jipya, kwani limekuwa likitokea mara kwa mara, hasa nyakati za mvua. Si Jangwani pekee, athari zilishuhudiwa hata katika maeneo mengine, ikiwamo daraja la Kigogo ambalo nalo halikuwa linapitika, wanaoishi pembezoni mwa Mto Msimbazi pia walikuwa hatarini.

Baadhi ya wananchi walishuhudiwa wakihamisha samani na vifaa mbalimbali kupeleka maeneo salama, lakini wapo waliokimbilia maeneo yenye miinuko bila kuokoa chochote.

Mwandishi wa gazeti hili alishuhudia katika eneo hilo na mengine aliyopita athari za mvua hizo zinazoendelea kunyesha. Eneo la Jangwani lilifungwa na utepe kuashiria hatari na kutoruhusu chombo chochote cha usafiri kupita, huku polisi wakipita huku na kule kufanya doria.

Hakukuwa na anayeweza kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine, hali iliyosababisha magari yaliyotoka Posta na Kariakoo, safari zao ziliishia Kituo cha Fire, huku zile zinazoingia zinaishia Magomeni Mapipa.

Haikuwa kama kawaida ya siku zote, kwamba kunakuwepo wale wanaovusha watu, hali ya jana haikuruhusu hilo kutokana na mafuriko hayo. Changamoto hizo, zilisababisha wananchi waibue hoja ya umuhimu wa kuharakishwa kwa mradi wa barabara za juu kutoka Magomeni Mapipa hadi Fire, kama anavyoeleza Simon Elia, mmoja wa wananchi hao. “Hii ni aibu, kila mvua ikinyesha usafiri unakuwa mgumu katika eneo hili. Kwa nchi inayojipanga kukuza uchumi wake ni muhimu ikaangalia namna ya kufanikisha ujenzi wa daraja hilo kwa kuwa hii ni njia kubwa na wengi wanaitumia,” alisema. Malensiana Nyoni, mfanyabiashara wa usafiri mtandaoni alisema taarifa za kufungwa kwa daraja hilo zinasababisha hasara kwao, wengi waliahirisha safari na kubaki nyumbani baada ya kusikia daraja halipitiki.

“Ni muhimu kwa nchi iliyojidhatiti kuleta maendeleo kuyatupia maeneo yenye changamoto kuboresha miundombinu yake kupitike kirahisi, kwa kuwa kodi zinazotumika kujenga zinatoka kwa wananchi,” alisema.

Kisiwani Zanzibar ambako kulitokea mafuriko, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Hamza Hassan Juma alisema wanaendelea kufanya utafiti kubaini ukubwa wa tatizo hilo. “Ninachotaka kusema kama Serikali suala hili la uwepo wa mvua kubwa tulisema miezi miwili nyuma na kuwataka watu wajiandae kuhama maeneo yao, lakini watu walikaidi taarifa hiyo,’’ alisema.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Makame Khatib, mvua zinazoendelea kunyesha Zanzibar zimesababisha familia 2,440 kukosa makazi baada nyumba zao kuingia maji yaliyosababishwa na mvua hizo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live