Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hiki ndicho kinaitofautisha Dodoma na Dar kimapato

9860 Pic+dodoma TanzaniaWeb

Fri, 3 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma/Dar. Ni kwa nini Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na lile la Dodoma yana tofauti za mapato?

Hili ni swali lililoibua mjadala baada ya Rais John Magufuli katika matukio tofauti kutoa takwimu zinazoonyesha Dodoma inaongoza kwa mapato kati ya majiji sita yaliyopo nchini, likiizidi Dar es Salaam.

Imeelezwa kinachosababisha tofauti ya mapato kati ya majiji hayo ni muundo wake, idadi ya watu na vyanzo vya mapato vilivyopo.

Kwa mara ya kwanza Rais Magufuli alizungumzia mapato hayo mwishoni mwa Julai, Ikulu jijini Dar es Salaam alipokabidhi hati miliki za viwanja kwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yenye makazi yake nchini kwa ajili ya kujenga ofisi na makazi katika makao makuu ya nchi jijini Dodoma.

Juzi, Rais alirejea kauli hiyo Ikulu alipozungumza na wakuu wa mikoa baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua.

Rais alisema kati ya majiji yote, Dodoma linaongoza kwa makusanyo ya mapato ya Sh24.2 bilioni ikiwa ni asilimia 123 ya makisio yao ya Sh19 bilioni.

Alisema Jiji la Dar es Salaam ambalo ni kongwe kuliko yote lilikusanya Sh15.3 bilioni, Arusha (Sh10.3 bilioni), Mwanza (Sh9.3 bilioni), Tanga (Sh9.1 bilioni) na Mbeya (Sh4.2 bilioni).

Kwa nini Dodoma

Mauzo ya viwanja na vyanzo vya mapato vilivyokuwa chini ya iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ndivyo vimelipa sifa jiji hilo kwa kuongeza makusanyo maradufu.

Mkurugenzi wa jiji, Godwin Kunambi akizungumza na Mwananchi juzi, alisema katika mwaka wa fedha wa 2017/18 walivuka lengo la makusanyo kwa asilimia 120.

Alisema mwaka 2017/18 walipanga kukusanya Sh20.8 bilioni kama vyanzo vya ndani vya mapato, lakini hadi Juni 30 walikusanya Sh25.1 bilioni. Alisema Sh19.5 bilioni zilitumika.

Kunambi alisema vyanzo vya mapato ni uuzwaji wa viwanja ambao awali ulikuwa ni jukumu la CDA.

Mamlaka hiyo ilivunjwa na Rais Magufuli, Mei 15, mwaka jana na ilitakiwa kukabidhi mali na madeni yote kwa iliyokuwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ambayo sasa ni jiji.

Kunambi alisema baadhi ya watumishi wasio waaminifu walikuwa wakikadiria mapato kidogo ili wakusanye na kuonekana wamevuka lengo, tatizo ambalo walikabiliana nalo.

Alisema matumizi ya mashine za kutoa risiti za kielektroniki (EFD) yameongeza makusanyo kwa kiasi kikubwa. Pia, zimeongeza imani ya wafanyabiashara kwamba wanalipa kodi kwa Serikali badala ya kuingiza mifukoni mwa watu.

Taarifa za jiji hilo zinaonyesha kuwa, mwaka 2014/15 iliyokuwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ilipanga kukusanya Sh3.9 bilioni, lakini ilikusanya Sh2 bilioni.

Mwaka 2015/16 ilipanga kukusanya Sh4.6 bilioni, hata hivyo ilikusanya Sh3.7 bilioni sawa asilimia 80.28.

Katika mwaka wa fedha wa 2016/17 Dodoma ilitarajia kukusanya Sh3.9 bilioni lakini ilivuka lengo kwa kukusanya Sh4.8 bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 123.

“Rais aliniteua kuwa mkurugenzi wa manispaa Septemba 13, 2016, nilikuta utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2016/17 ya Sh3.9 bilioni. Niliendelea kutekeleza bajeti ambayo sikuanza nayo lakini tukavuka lengo,” alisema Kunambi.

Katika kikao cha baraza la madiwani cha kufunga mwaka juzi, Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe alisema pamoja na pongezi na sifa nyingi walizomwagiwa hata na Rais, iko haja ya kujitathmini kuhusu vyanzo hivyo.

Profesa Mwamfupe alisema chanzo cha ardhi kisiwe tegemeo kubwa kwa kuwa haidumu mikononi mwao na suala la viwanja ni la kupita kwa msimu.

“Pamoja na kuwa tumepata mapato mengi bado ninasisitiza wataalamu kutembelea maeneo yetu yote ili mkatafute na kubuni vyanzo vipya, leteni na mbinu za kukusanya kwa urafiki na wadau bila ya kuwaumiza. Tujenge vitega uchumi sasa ili tusirudi nyuma,” alisema Profesa Mwamfupe.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Dodoma Mjini, Robert Muwinje aliwataka madiwani kuwa wabunifu katika vyanzo vya mapato kwa kuwa suala la viwanja lina mwisho wake na ukifika wanaweza kujikuta hawana kitu.

Muwinje alisema ni wakati wa kufanya kazi kwa kushirikiana kati ya madiwani na watumishi lakini kikubwa wajenge dhana ya kuaminiana na kusameheana kwa kuwa wote ni binadamu.

Hali Dar es Salaam

Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, alisema Jiji la Dar es Salaam haliwezi kamwe kupitwa kimapato na Jiji la Dodoma.

Jacob ambaye ni mjumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, alisema kuna tofauti za kimuundo kati ya Dar es Salaam lenye watu milioni tano na Dodoma lenye watu milioni mbili. Mkoani Dar es Salaam, jiji ni mojawapo ya halmashauri sita; zingine zikiwa ni Kigamboni, Temeke, Ubungo, Kinondoni na Ilala. Dodoma ina halmashauri moja tu ya jiji.

Jacob alisema Halmashauri ya Manispaa ya Ilala katika bajeti ya mwaka 2017/18 ilipanga makusanyo ya Sh46.6 bilioni na ilikusanya Sh44.5 bilioni sawa na asilimia 95.5

Alisema Kinondoni mwaka 2017/18 ilipanga kukusanya Sh31.6 bilioni, lakini ilikusanya Sh29.7 bilioni sawa na asilimia 94 wakati Ubungo ikikadiria kukusanya Sh16.5 bilioni, lakini ilikusanya Sh13.5 bilioni sawa na asilimia 81.8

Jacob alisema Jiji la Dar es Salaam mwaka 2017/18 lilipanga kukusanya Sh16.4 bilioni, lakini lilikusanya Sh16.8 bilioni sawa na asilimia 102.

Alisema Manispaa ya Temeke, ilipanga kukusanya Sh30.9 bilioni, lakini ikakusanya Sh29.03 bilioni sawa na asilimia 94, wakati Kigamboni ikilenga kukusanya Sh9.2 bilioni na makusanyo yakawa Sh5.5 bilioni sawa asilimia 59.

Alisema halmashauri zote za Dar es Salaam zilipanga kukusanya Sh151.3 bilioni na zikakusanya Sh139.1 bilioni sawa na asilimia 91.95.

“Kiasi hiki cha fedha ndicho kimechangiwa na watu milioni tano wa Dar es Salaam sasa ndipo ulinganishe na mapato yote ya Jiji la Dodoma waliopata Sh24.4 bilioni kwa makusanyo ya watu milioni mbili,” alisema Jacob.

Meya Jacob alisema anakubaliana na Rais kuwa kuna ‘upigaji’ wa mapato katika halmashauri.

Alisema Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo anafahamu wanavyopambana kuzuia mianya ya ubadhirifu wa mapato ya halmashauri.

“Ni utaratibu mzuri wa Rais kulinganisha na kushindanisha mapato ya halmashauri nchi nzima. Utaratibu huu unafanya tupambane kuwa vinara wa ukusanyaji mapato,” alisema Meya Jacob ambaye aliwapongeza Dodoma na Ubungo kufanya vizuri kwa mara ya kwanza.

Diwani wa Tabata (Chadema), Patrick Assenga alisema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inakusanya mapato mengi licha ya kuwa na vyanzo vichache ambavyo havizidi vitano.

“Vyanzo hivyo ni ushuru wa maegesho ya magari, ushuru wa stendi ya mabasi Ubungo na Machinga Complex. Vyanzo vingine vinakusanywa na halmashauri husika ikiwamo leseni za biashara na ushuru wa masoko,” alisema Assenga.

Alisema kauli ya Rais ni kama inazilenga halmashauri zinazoongozwa na upinzani kwamba hazifanyi vizuri katika kutekeleza majukumu yake.

Mjumbe wa Baraza la Madiwani la Jiji la Dar es Salaam ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini, alisema chini ya uongozi wa Mkurugenzi wa jiji hilo, Sipora Liana akishirikiana na Meya Isaya Mwita wamejitahidi kuongeza mapato kutoka Sh6 bilioni miaka iliyopita hadi kufikia Sh16 bilioni za sasa.

Alisema tofauti na Dar es Salaam, Dodoma ina vyanzo vya mapato ya ndani vipatavyo 30 ukiwamo ushuru wa hoteli na viwanja.

Chanzo: mwananchi.co.tz