Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hiki ndicho kinachoitesa Kigoma Ujiji hadi kupata hati chafu mfululizo

26667 Pic+ujiji TanzaniaWeb

Tue, 13 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Matumizi ya Sh900 milioni za Benki ya Dunia (WB) kinyume na utaratibu katika Manispaa ya Kigoma Ujiji kumeifanya iingie matatizoni kwa kupata hati chafu mara nne mfululizo.

Fedha hizo ambazo zilipelekwa na WB mwaka 2012 zilikuwa kwa ajili ya mradi wa uendelezaji wa mji lakini manispaa hiyo ilizihamishia kwenye ujenzi wa maabara ya shule za sekondari bila kufuata utaratibu.

Maelezo yaliyotolewa na Meya wa Kigoma Ujiji, Hussein Ruhava alipohojiwa na Mwananchi mkoani humo kujua chanzo cha manispaa hiyo kupata hati chafu mara nne mfululizo, alisema matumizi mabaya ya fedha na uzembe ndiyo yaliyosababisha hali hiyo.

“Tunao mradi wa Benki ya Dunia ulioanza kutekelezwa mwaka 2012, kulikuwa na fedha zinazofikia Sh777 milioni ambazo hazikujulikana matumizi yake. Tulipouliza tuliambiwa zimetumika kujenga maabara za shule za sekondari,” alisema Ruhava.

Alisema ujenzi huo ulitokana na agizo la Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete aliyetaka kila shule ya sekondari ya kata iwe na maabara.

Mbali na miradi ya WB, Ruhava alisema kulikuwa na fedha za Mfuko wa Barabara (Road Fund) zaidi ya Sh200 milioni lakini walipouliza nazo waliambiwa zimeelekezwa kwenye ujenzi wa maabara.

Aliitaja miradi iliyotakiwa kutekelezwa na fedha za Benki ya Dunia kuwa ni ujenzi wa barabara, dampo la kisasa na machinjio.

Alisema licha ya kutumia fedha hizo shule zilizokamilisha ujenzi wa maabara ni tatu kati ya 19.

Ruhava alisema kuwa kitendo cha watendaji wa manispaa kuhamisha fedha za miradi hiyo kwenye miradi

mingine kilikuwa moja ya sababu za kupata hati chafu. Alisema licha ya miradi iliyokusudiwa na Benki ya Dunia kukamilika, bado mkandarasi alikuwa akiidai manispaa Sh777 milioni.

Kwa mujibu wa Ruhava, ili kunusuru miradi mingine walilazimika kukopa Sh1.1 bilioni kutoka Benki ya NMB ili kulipa deni la mkandarasi na kukomboa jengo la Shirika la Maendeleo la Kigoma (Kigodeco) lililochukuliwa na Benki ya CRDB ambayo nayo ilikuwa ikiwadai Sh370 milioni. Kutokana na mkopo huo alisema sasa fedha zote wanazopata wanalipa benki hivyo kusimamisha miradi ya maendeleo.

Maabara zilijengwa?

Meya Ruhava, alisema shule zilizojengewa maabara na kukamilika ni tatu kati ya 19. Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi katika shule zilizokamilika ulibaini kuwapo changamoto kubwa.

Miongoni mwa shule zilizojengewa maabara ni Shule ya Sekondari ya Kasingirima iliyopo Ujiji. Katika shule hiyo kumejengwa maabara tatu lakini moja tu ya Fizikia ndiyo iliyokamilika na kuanza kutumika.

Mkuu wa shule hiyo, Venance Ndegeya alipoulizwa kuhusu maabara hizo shuleni hapo aliliambia Mwananchi kuwa alipokea Sh25 milioni kutoka ofisi ya mkurugenzi wa manispaa mwaka 2014 ambazo alijengea maabara tatu hadi hatua ya kupaua.

“Kwa hiyo shule ilipokea Sh25 milioni kutoka kwa mkurugenzi kwa ajili ya ujenzi wa maabara za Baiolojia, Fizikia na Kemia, lakini maabara hizo hazikukamilika bali zilifikia hatua ya upauaji tu,” alisema.

Alisema maabara hizo hazikuweza kutumika hadi ilipofika 2018. “Ilipofika Februari 2018 tulipokea fedha kutoka Mfuko wa Education Program for Results (EP4R) Sh9.1 milioni, tuliweka vipaumbele na ofisa elimu ili maabara moja itumike. Tukachukua chumba cha Fizikia kilichojitenga, tukaweka sakafu, meza, madirisha ya aluminiam, mfumo wa maji, rangi na milango”.

Hata hivyo, alisema walishindwa kumalizia kuweka umeme na mfumo wa gesi kwa sababu fedha ziliisha. Kwa sasa wanatumia majiko ya mafuta ya taa katika maabara hiyo kwa kuwa wanasubiri fedha nyingine kutoka manispaa.

Hatua gani zimechukuliwa?

Mkurugenzi Mtendaji wa manispaa hiyo, Mwaliwa Pangani aliliambia Mwananchi mjini Kigoma kuwa kutokana na matumizi ya fedha hizo kubadilishwa amewasimamisha kazi watumishi wanne, ambao ni mweka hazina, ofisa ununuzi, mkaguzi wa ndani na aliyekuwa kaimu mkurugenzi mtendaji. “Wameshajieleza wote kwa hiyo tunataka kuunda timu kwa ajili ya kuchunguza maelezo yao,” alisema Pangani.

Hati chafu

Kuhusu manispaa hiyo kupata hati chafu mfululizo Pangani alisema ni pamoja na kukiuka utaratibu wa kifedha na maelekezo ya CAG au udhaifu katika ufungaji wa vitabu. “Usipofuata maelekezo ya CAG lazima utapata hati chafu, japo si rahisi kuipata. Sababu hasa za kupata hati chafu ni kwanza halmashauri ina madeni makubwa mengi, halafu fedha nyingi zilirukwa,” alisema.

Akifafanua sababu nyingine za kupata hati chafu, Diwani wa Kata ya Rubuga (Chadema), Omari Gindi alidai tatizo ni mfumo wa uendeshaji wa Serikali. “Unajua unapofika wakati wa uchaguzi, kuanzia Juni 31, mwaka wa uchaguzi, Baraza la Madiwani huwa halipo. Anabaki mkurugenzi na watendaji wake. Hapo ndipo madudu yanapofanyika,” alidai Gindi.

Alitaja sababu ya pili ya hati chafu kuwa ni ofisi ya mkurugenzi kutopeleka kitabu cha hesabu kwa CAG licha ya baraza la madiwani kukipitisha. Hati chafu ya tatu ilisababishwa na kutojibiwa kwa hoja za CAG na kutoonekana kwa viambatanisho.



Chanzo: mwananchi.co.tz