Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hifadhi ya Ngorongoro inavyowajengea uwezo wafugaji nyuki, wananchi

F3cebef78d64b6f8d867901ddc9778f1.png Nyuki

Tue, 21 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

UHUSIANO uliopo kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi hiyo, unachangiwa kwa kiasi kikubwa na uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati.

Sheria iliyoanzisha Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro lenye matumizi mseto ya ardhi kwa wanyamapori, binadamu na mifugo katika eneo moja inazuia kufanya baadhi ya shughuli za kiuchumi kama vile kilimo na ujenzi wa nyumba za kudumu kwa wananchi katika eneo hilo. Hizo ni shughuli ambazo zingesaidia ustawi wa jamii kwa kiasi kikubwa.

Kwa kulitambua hilo NCAA, imekuwa ikichangia miradi mbalimbali ya kijamii ili kuwawezesha wananchi kiuchumi. Miradi hiyo inahusisha uundaji wa vikundi vya ufugaji nyuki vinavyojihusisha na urinaji wa asali pamoja na mazao yatokanayo na nyuki; na kusaidia vikundi vya akina mama wanaojihusisha na kazi za kiutamaduni kama vile utengenezaji wa shanga.

Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Dk Freddy Manongi anabainisha kuwa, utalii hauwezi kuwa na manufaa kama hausaidii maendeleo ya wananchi hasa wanaoishi na kuendesha shughuli zao katika Hifadhi ya Ngorongoro.

Hii ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano kupitia mamlaka hiyo, imekuwa ikitumia sehemu ya mapato yake kusaidia miradi mbalimbali ili kuimarisha hali ya maisha ya wananchi.

Dk Manongi anaongeza kuwa, utekelezaji wa miradi ya kusaidia vikundi vya ufugaji nyuki pekee umeshanufaisha wananchi 374 kutoka kata 14 ambao kupitia programu hiyo, wananchi walionufaika na elimu ya ufugaji nyuki wamekuwa viongozi na walimu wa kuwafundisha wenzao katika vijiji mbalimbali.

Kupitia programu maalumu za elimu kwa wafugaji nyuki imewasaidia kujua njia bora ya ufugaji nyuki, urinaji wa asali, vifungashio safi na salama vya asali na njia bora za kupanua masoko kipitia maonesho mbalimbali na mikutano ya kimataifa inayofanyika nchini.

Anafafanua kuwa, kati ya Mwaka wa Fedha 2015/2016- hadi 2019/2020 Mamlaka hiyo imetumia takribani Sh 213,985,000 kusaidia vikundi vya ufugaji nyuki kwa kuwanunulia mizinga 1900.

Aidha, zimetumika kuwapa elimu ya ufugaji nyuki na kuwapeleka katika maonesho makubwa kama Sabasaba na sikukuu za wakulima na wafugaji maarufu kama Nanenane ili kuonesha bidhaa zao na kujipanua katika masoko mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Katika kipindi hicho, Hifadhi ya Ngorongoro imetoa Sh 62,995,000 kwa ajili ya kusaidia vikundi vya akina mama wanaotengeneza shanga na vitu vingine vya kiutamaduni ambavyo vimekuwa sehemu ya utalii ndani Hifadhi ya Ngorongoro.

“Tunafanya haya kwa kuwa sheria iliyoanzisha mamlaka hii inazuiya baadhi ya shughuli kufanyika ndani ya hifadhi, ndiyo maana Serikali kupitia NCAA tunasaidia jamii hii ili kuwapunguzia ukali wa maisha kwa kiwango fulani,” anasema Dk Manongi.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia Idara ya Maendeleo ya Jamii, Fedes Mdalla, anasema katika utekelezaji wa miradi ya ufugaji nyuki, NCAA imeratibu uanzishwaji wa vikundi 25 katika kata 11 za Tarafa ya Ngorongoro na kuhakikisha kuwa vikundi hivyo vinapewa mafunzo ya ufugaji nyuki.

Mengine ni mafunzo ya utundikaji mizinga, urinaji asali unaojali mazingira, vifaa vya kurina asali, namna ya kuhifadhi asali, uchakataji wa mazao ya nyuki, ubora wa asali, vifungashio na masoko, aina za asali na matumizi yake na utambuzi wa asali bora kwa njia za asili.

Mdalla anaongeza kuwa, lengo la Mamlaka ni kuviongezea vikundi vya nyuki uwezo wa kuzalisha asali kwa wingi, ili kukidhi mahitaji ya kiwanda cha asali kinachotarajiwa kujengwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kama kitega uchumi kwa wenyeji kupitia biashara ya asali katika masoko ya ndani na nje ya Mamlaka.

Anataja vikundi vinavyonufaika na mradi wa ufugaji nyuki kuwa ni Nyuki Olbalabal, Naserian, Nyangulo Group, Napokieki, Enaboishu, Naserian Irmutende, Kikundi cha Nyuki Embarway Group na Eretet Losilale. Vikundi vingine vilivyonufaika na ufugaji huo wa nyuki ni Namunyak Madukani, Ireteti Honey Making, Kikundi cha Sinoni, Nasaru, Naboishu, Meroyo, Kidemi, Matonyok, Naretoi, Namelok, Naramatisho, Ramat, Kinyok, Namayana, Nabulaa, Kipok, Nadupoi, Naning’o, Nasinya na Beshta.

Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Jamii wa NCAA, Bashir Nchira anabainisha kuwa, kati ya mwaka 2015 na 2019, Mamlaka hiyo imeshatoa mizinga ya nyuki 1900 kwa vikundi 25 ili kuongeza tija ya uzalishaji wa asali na kupandisha mnyororo wa thamani kwa mazao ya nyuki na bidhaa nyingine za kitamaduni hasa kwa wenyeji ndani ya hifadhi.

“Kwa mfano, mwezi Mei 2020, tumegawa mizinga 400 kwa vikundi hivyo 25; sambamba na mizinga hiyo, tumewapa na vifaa vingine vya kurina na kufungasha asali kama vile, kopo za kufungashia, buti, ovaroli, kofia na chujuo la asali,” anasema.

Nchira anaongeza: “Tunaamini baada ya muda, uzalishaji utaongezeka sana ndiyo maana serikali kupitia Hifadhi ya Ngorongoro iko katika mipango ya ujenzi wa kiwanda hicho na tunaamini wazo hili litasaidia kuunganisha shughuli za ufugaji na utalii ili kutangaza utalii wa Ngorongoro kama sehemu ya kipekee duniani.”

Baadhi ya wanufaika wa mizinga ya ufugaji nyuki akiwemo Theresia Kamyanda kutoka Kata ya Ngorongoro, anasema zamani wanawake wa Kimasai katika eneo hilo walitegemea kazi za kutengeneza shanga na kuuza maziwa kwa watumishi wa NCAA, lakini miradi ya ufugaji nyuki imewasaidia kuongeza kipato kutokana na mauzo ya asali.

“Ni jambo la kushukuru sana, sisi akina mama wa Kimasai hatulimi, lakini utaratibu wa kupewa mizinga pamoja na elimu ya ufugaji nyuki na namna bora ya kurina asali imetusaidia sana kupata asali ambayo tunauza kuanzia 10,000 kwa chupa. Hii inatusaidia sana kwa mahitaji yetu hasa chakula kwa familia zetu,” anasema Theresia.

Naye Mzee Ngenyikei Mollel wa Kata ya Olbalbal, anaipongeza Serikali kwa kuwepo na Idara ya Maendeleo ya Jamii ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kwani kila mwaka imekuwa ikishirikiana na wananchi kubuni miradi endelevu inayosaidia ustawi wa maisha yao na kupunguza utegemezi kwa kiasi kikubwa.

“Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa inasaidia wanyonge sana, tunalishuhudia hili kwa vitendo kwa kuwa mbali na uboreshaji wa huduma za elimu, afya na maji, tumekuwa tukipata elimu ya kubuni miradi ya kiuchumi kwa wananchi kama hii ya ufugaji nyuki; kuna vikundi vya ushirika hapa Ngorongoro mfano kule Ngoile ambako wanakikundi wamefikisha mtaji wa zaidi ya Sh milioni 7 na hii yote isingewezekana bila NCAA kuweka mkono wake.”

Mwandishi wa makala haya ni Ofisa Uhusiano katika Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Chanzo: habarileo.co.tz