Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hifadhi Mlima Rungwe  ilivyowakosha Wabunge

Fd15065fc4b9fdb44a8678dca0c27e52 Hifadhi Mlima Rungwe  ilivyowakosha Wabunge

Fri, 9 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

“ASANTE kwa kutembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Mlima Rungwe. Karibu tena,” ni maneno ambayo walijikuta wakiyasoma mara kwa mara wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii walipowasili kituo cha mapumziko cha Kandoro Camp, baada ya kupanda mlima Rungwe uliopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Ni maneno waliyoyatamka wakisoma kutoka kwenye ngao walizotunukiwa, ikiwa ni ishara ya shukrani na pongezi kwa kupanda mlima huo. Kila mgeni anayetembelea hifadhi na kupanda mlima huo hupewa ngao hiyo.

Mlima Rungwe ni mlima wa tatu kwa urefu nchini nyuma ya mlima Meru unaoshika nafasi ya pili baada ya Mlima Kilimanjaro ambao ni wa kwanza kwa urefu, si Tanzania pekee bali Afrika nzima.

Mazingira ya uoto wa asili yanaufanya mlima huu siyo tu uwe na mwonekano mzuri wenye ukijani wa kudumu bali pia kuwa kivutio kikubwa cha utalii katika ukanda wa eneo la Nyanda za Juu Kusini.

Ni uoto huu wa asili ambao huwavutia wanyama wa kipekee kama Kipunji na Mbega kuishi, huwavutia watafiti kwenda kufanya shughuli zao lakini hata watalii wanaofika hapa hawachoshwi na madhari nzuri ya hifadhi hii.

Hicho ndicho kilichowafanya pia wajumbe wa kamati hii ya Bunge kujikuta wakitamani waendelee kukaa mlimani humo licha ya kuwepo kwa wingu zito lililokuwa limetanda likiashiria kwamba mvua ingeweza kunyesha wakati wowote kama ilivyo kawaida ya hali ya hewa ya wilaya ya Rungwe.

Uwepo wa kuvutia wa uoto asilia wa Mlima Rungwe unatokana na juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuyatunza mazingira haya.

Serikali chini ya Wakala wa Misitu nchini (TFS) imeendelea kusimamia utunzaji wa mazingira na kuufanya mlima huu na eneo lake lote kuzidi kuwa kivutio, hatua iliyosababisha wajumbe wa kamati kupongeza juhudi zinazofanyika.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Aloyce Kwezi ni miongoni mwa wabunge walioonesha kuvutiwa sana na mandhari ya Mlima Rungwe. Anasema ipo haja ya kuongeza juhudi katika kuyalinda na kuyatunza mazingira hususani msitu wa miti ya asili unaoufunika mlima huu.

“Kwanza tunapenda kusisitiza wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wahifadhi, watunze misitu yote ambayo tunayo. Tuache zile tabia za kuchoma moto misitu. Lakini jambo la msingi zaidi naomba tuimarishe utalii wa kutembelea katika misitu. Tumekariri kwamba utalii mzuri ni wa kwenda kuangalia wanyama, mito na vitu vingine.

“Lakini tunajisahau kwamba hii misitu hapa tuliposimama ndiyo chanzo cha Mtera, ndiyo chanzo cha maji kinapeleka Bwawa la Umeme la Nyerere. Jambo la msingi ni kutunza misitu hii ili tuendelee kupata umeme wa kutosha, tuendelee kuwa na maji safi, tuendelee kuenzi urithi wa vizazi vitakavyokuja. Misitu hii ni hewa nzuri kama mnavyoiona lakini pia ni hifadhi ya viumbe wakiwemo wanyama kama tulivyowaona.”

Anaendelea kusema: “Mimi niombe uhifadhi wa misitu uendelee na pengine nichukue nafasi hii kuendelea kuipongeza Wizara ya Maliasili na kukupongeza sana Profesa (Dos Santos) Silayo (Mtendaji Mkuu wa TFS). Kwa kweli usimamizi wako wa misitu ndiyo matokeo mazuri tunayoyaona hapa.”

Dk Kwezi anautaka uongozi wa wilaya na halmashauri kuhakikisha wanawatumia maofisa watendaji na wenyeviti wa vijiji kutoa elimu ya umuhimu wa kuendelea kuitunza hifadhi hiyo ikiwemo kuwabaini watu wanaoanzisha moto kama ilivyotokea mwaka jana ambapo moto uliteketeza sehemu kubwa ya eneo la msitu.

“Ni muhimu tukatambua kuwa ni hifadhi hii hii ya Mlima Rungwe inazalisha maji yanayokwenda kuzalisha umeme kwenye mabwawa yetu makubwa tunayoyategemea. Yanajaza kule Mtera na ndiyo yanategemewa hata kwenye mradi mkuwa wa bwawa la Mwalimu Nyerere. Hivyo hifadhi hii hainufaishi watu wa Mbeya pekee bali Tanzania yote,” anasema.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja anasema ni muhimu watanzania kutambua umuhimu wa kutunza maliasili ya misitu kutokana na umuhimu wake kwa viumbe hai vilivyopo na vijavyo.

“Kwanza misitu ni uhai, ni vyanzo vya maji. Lakini misitu pia ni sehemu mojawapo ya tiba mbadala kwenye miili yetu. Hata leo hii tulivyofika katika msitu huu, utaona kabisa kwa kiasi flani afya zetu zimeimarika.Niwahamasishe watanzania kwamba maeneo ya misitu ni maeneo muhimu sana. Yanatuletea mvua, yanatunza vyanzo vya maji na kuleta hali ya hewa nzuri,” anasema.

Anasema maeneo yanayonyemelewa na jangwa ni yale ambayo watu wake walikata sana miti ikiwa ni pamoja na mikoa ya kanda ya ziwa.

“Ukizingatia mimi natokea kanda hiyo (ya Ziwa) nina wahamasisha sana watanzania wote waliopo kwenye maeneo yanayofanana na mkoa wa Mwanza wajifunze kwamba kutunza misitu ya asili ni muhimu sana na ni sehemu ya kuleta maendeleo katika nchi yetu.

“Ukiangalia hali ya huku iko tofauti sana na ile iliyopo Kanda ya Xiwa. Hali ya huku imetulia vizuri, mandhari nzuri inavutia. Tuone umuhimu wa kutunza misitu ya asili kama urithi maridhawa wa nchi yetu kwani misitu pia kivutio cha watalii.

Kamishina wa uhifadhi wa wa misitu nchini, Profesa Silayo anasema ni jambo la kufurahisha kutembelewa na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwenye mazingira asilia ya hifadhi ya Mlima Rungwe.

“Bunge kama mhimili muhimu katika nchi yetu unaotunga sheria, kuja kwao hapa kunawapa fursa pana ya kuona fursa na umuhimu wa misitu na hivyo mtachangia vizuri zaidi katika kujenga misingi ya kuwa na sheria ambazo zitaimarisha hifadhi za misitu yetu na maliasili kwa ujumla.

“Mmeona msitu huu umetunzwa vizuri sasa ni rai yangu kwa wananchi wanaozunguka msitu huu kuendelea kuutunza vizuri. Na si hapa tu tunatoa rai kwa wananchi nchini kote kuendelea kutunza Hifadhi za mazingira za misitu asilia walizonazo,” anasema.

Chalya Julius, mkuu wa Wilaya ya Rungwe, anaitaja hifadhi hii ya Mlima Rungwe kuwa kitovu na chemichemi inayounufaisha mkoa mzima wa Mbeya.

Chalya anasema pamoja na changamoto zilizopo kwa baadhi ya wakazi wa maeneo jirani kuvamia hifadhi hiyo, wapo baadhi ya wananchi wanaoonesha nia ya kuendeleza utunzaji mazingira kwa kupanda mazao mbalimbali ya miti ikiwemo ya maparachichi.

Anasema ingawa wanapanda kwa ajili ya biashara ya zao hilo upande wa utunzaji mazingira nao unanufaika kwa uhifadhi kupitia misitu ya miti hiyo.

Hata hivyo, mkuu huyo wa wilaya anasema ipo changamoto ya usafiri kutoka eno la barabara kuu hadi milango ya kuingilia kwenye hifadhi hiyo kutokana na ubovu wa barabara na kwamba inapunguza watalii kutembelea eneo hilo.

“Nadhani mmejionea wenyewe kutoka eneo la barabara kuu mpaka kufika hapa lango la Syukula. Ubovu wa barabara unaweza kusababisha mtu akija mara moja asitake kurudi tena au kushawishi wengine,” anasema Chalya.

Kwa angalizo hilo wabunge hao waliahidi kulisemea Bungeni na kuishauri Serikali kujenga barabara hiyo.

Mhifadhi wa hifadhi asilia ya mazingira ya Mlima Rungwe, Yusuph Tango anasema ipo mito tisa inayoanzia Mlima Rungwe kwenda moja kwa moja ziwa Nyasa huku msitu wa Poroto ulio ndani ya Hifadhi hiyo eneo la Ziwa Ngosi ukiwa na mito mitano inayotiririsha maji yake kwenda mto Songwe unaopeleka maji yake Ziwa Rukwa.

“Kwa hiyo unaweza ukaona ni jinsi gani maeneo haya ni muhimu sana. Lakini pia hifadhi yetu hii ni kitovu cha mimea ikiwemo ya kipekee wake. Yupo nyani anaitwa Kipunji ni jamii mpya ya nyani, mwanzoni alionekana ni nyani wa kawaida baadaye watafiti kutoka WCS wakaja na majibu kuwa ana utofauti sana na nyani wengine na kwa mara ya kwanza aligundulika kwenye mlima huu,” anasema Tango.

Wabunge wanasema mazingira ya Hifadhi ya Msitu Asilia wa Mlima Rungwe wanashauri kwamba sambamba na kuongeza umakini katika uhifadhi wake pia wanasema inapaswa kutumika kwa maonesho na mashindano mbalimbali ikiwemo Mbio za Marathon kwa ajili ya kuutangaza zaidi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz