Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hiace zilizogongana uso kwa uso zateketeza 16 kwa moto

Tue, 27 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tarime. Hadi sasa watu 16 wamethibitishwa kufariki dunia katika ajali ya magari wawili aina ya Hiace kugongana uso kwa uso jana kisha kuwaka moto katika barabara kuu ya Musoma- Mwanza-Tarime.

Ajali hiyo iliyotokea katika kijiji cha Komaswa wilayani Tarime mkoa wa  Mara ambapo mbali na vifo hivyo watu watatu wamejeruhiwa vibaya na wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga amesema hadi sasa chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana lakini polisi wanafanya uchunguzi.

Luoga amesema baada ya magari hayo kugongana yaliwaka moto na kuunguza abiria pamoja na mizigo iliyokuwapo ndani huku miili 15 ikitolewa ikiwa imeungua vibaya kwa moto.

Amesema watu wanne waliokolewa wakiwa wamejeruhia lakini mmoja alifariki njiani akiwa anapelekwa kwenda Bugando kwa matibabu.

Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha magari hayo yaligongana baada ya madereva ambao wote walifariki kwenye ajali hiyo kushindwa kuona mbele kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha wakati huo.

Amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Tarime kwa ajili ya taratibu za utambuzi na mazishi.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amesema Serikali mkoani humo inapanga namna gani mazishi ya marehemu hao yatafanyika.

Amesema mbali na kuzikwa kwa marehemu hao, lakini utaratibu unafanyika ili kuzoa mabaki na majivu ya miili yaliyopo katika eneo la tukio ili yaweze kuhifadhiwa vizuri kwa mujibu wa mila na taratibu kwani wana amini kuna mabaki ya watu walioungua katika ajali hiyo.

Amesema atatoa taarifa juu ya utaratibu wa mazishi baada ya kufanya kikao na wakuu wa wilaya za Tarime na Rorya.

Malima amesema hadi sasa miili mitatu imetambulika huku mingine ikiwa imeungua sana kiasi kwamba haiwezekani kutambulika ni jinsia gani.

Amesema miili iliyotambulika ni pamoja na wa dereva ambaye alitambulika kutokana na eneo alilokuwa amekaa na kwamba wakati mwili huo unatolewa kwenye gari uliwekewa alama.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz