Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hiace, bajaji kuondoa daladala za baiskeli barabarani

7e7eccd96370277b5da9db3780943302 Hiace, bajaji kuondoa daladala za baiskeli barabarani

Fri, 19 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

USAFIRI wa abiria kwa kutumia daladala za ‘hiace’ na ‘bajaji’ utaanza kutumika katika Manispaa ya Shinyanga, Aprili mwaka huu; Amesema Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Geofrey Mwangulumbi.

Kwa maana hiyo, usafiri uliokuwa umezoeleka wa daladala za baiskeli hautaruhusiwa kuingia katikati ya mji na uratibu wa hiace na bajaji utafanyika mwezi huu.

Mkurugenzi huyo aliyasema hayo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga baada ya madiwani kutaka usafiri wa uhakika uwepo ndani ya manispaa kama walivyoazimia katika vikao vya mwaka 2015 hadi 2020.

Alisema: “Usafiri wa hiace na bajaji utaanza Aprili kwani utaratibu unafanyika na njia zipo na vituo vya kusimama daladala vilikwishawekwa; wamiliki wataitwa katika kikao cha makubaliano ili usafiri huo uanze mara moja.”

Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila, alisema baada ya huduma ya daladala kuanza, baiskeli zinazobeba abiria hazitoruhusiwa kuingia katikati ya mji, badala yake zitaruhusiwa kuendelea kutoa huduma katika maeneo ya pembeni ya mji.

Diwani wa Kata ya Mwawaza, Juma Nkwabi, alitaka usafiri huo kuanza mara moja kwa kuwa mara nyingi imekuwa ikisemwa, lakini hakuna utekelezaji wake.

Mkazi wa manispaa hiyo, Salome Ndaki, alipongeza kuelekea kuanza kwa hatua hiyo ingawa watu walizoea usafiri wa baiskeli kuwabeba mpaka mlangoni mwa nyumba zao.

Chanzo: habarileo.co.tz