Helga Mchomvu, diwani wa Kata ya Muungano (Chadema) na mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Hai, ni miongoni mwa wanasiasa wanawake wanaochapa kazi vilivyo mkoani Kilimanjaro.
Halmashauri ya Wilaya ya Hai inaongozwa na Chadema baada ya kunyakua jata zote 17 katika Halmashauri hiyo katika Uchaguzi Mkuu 2015 na Mchomvu ndiye yuko nyuma ya uongozi huo. Hata hivyo, madiwani saba walijiuzulu katika vipindi tofauti na kujiunga na CCM.
Akizungumza na Gazeti hili, He Mchomvu ambaye pia ni katibu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Mkoa wa Kilimanjaro anasema aliingia katika chama hicho akiwa na lengo la kuwa sauti ya kinamama.
Changamoto za uongozi
Akizungumzia changamoto anazokabiliana nazo katika uongozi wake, Mchomvu anasema ya kwanza ni mtazamo wa baadhi ya watu kuwa mwanamke hawezi kusimama na kuwa kiongozi.
“...lakini ukweli ni kwamba mwanamke akiaminiwa na kupewa ridhaa anaweza na kufanya mambo makubwa ikiwa ni pamoja na kusimamia mambo kwa uaminifu mkubwa,” anasema.
Katika utendaji, Mchomvu anasema kikwazo kikubwa ni mwingiliano katika utendaji kazi na “hali ya siasa kuwa ngumu tofauti na miaka ya nyuma”.
Anaongeza, “Changamoto kubwa ni maingiliano katika utendaji wa kazi lakini pia utaratibu ambao hatukuuzoea tanbgu zamani wa kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa na kuhamasisha wanachama, kwa sasa tupo tu. Vitu ambavyo tulizoea kuvifanya miaka ya nyuma na kuimarisha chama, leo tumezuiwa,” anasema.
Anasema katika kipindi chake cha uongozi, amekutana na “biashara ya ununuzi wa madiwani” jambo ambalo anasema lilisababisha Chadema kupoteza Kata saba.
“Katika halmashauri yangu tulishinda kwa asilimia 100 katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, lakini baada ya muda kidogo ikaja biashara ya ununuzi wa madiwani na binafsi sitakaa nisahau hili maana ni kitu ambacho hakikuwa sahihi,” anasema.
Anaongeza kuwa, “...mbaya zaidi, walewale waliochaguliwa na baadaye kujiuzulu kutoka upinzani, walirudishwa kugombea kupitia CCM.
“Hili liliniumiza sana hasa ikizingatiwa kuwa kodi na rasilimali ndogo za wananchi badala ya kuzitumia kujenga barabara, shule, hospitali na kununua dawa, tulizitumia kurudia uchaguzi”
Madiwani wa Chadema waliojiunga na CCM waliondoka kwa awamu na baada ya uchaguzi kurudiwa, CCM ilishinda na kupata madiwani saba kati ya 17.
Pamoja na changamoto hizo, anasema hajakata tamaa, anajiamini na anaweza kuendelea kuiongoza halmashauri hiyo na kuwezesha wananchi kuyafikia maendeleo waliyoyatarajia.
“Sijawahi kukata tamaa ya siasa na siwezi kukata tamaa, licha ya misukosuko na suluba nyingi ninazokutana nazo. Bado ninajiamini na ninaweza kuwavusha wananchi.
“Tunapitia mahali pagumu sana. Siasa zimekuwa kama uadui tofauti na zamani, lakini ninaisimamia halmashauri kwa uaminifu mkubwa na ninaamini tutaendelea kufanya vizuri”
Katika halmashauri hiyo, Mchomvu anasema mbali na siasa, changamoto kubwa kwa sasa ni miundombinu ya barabara ambazo kwa sasa zinashughulikiwa na wakala wa ujenzi wa barabara mijini na vijijini (Tarura) na katika sekta ya elimu kuna upungufu wa madarasa, hivyo wanaendelea kuhamasisha wananchi kuchangia.
Diwani huyo anasema pia wamehamasisha wananchi kuendelea kushiriki ujenzi wa nyumba za walimu pamoja na maabara kwa shule za sekondari ili kuwezesha wanafunzi kusoma kwa vitendo.
Mwenyekiti huyo anawataka wananchi wa Hai kutambua kuwa wanahitajika kutoa michango mbalimbali kwenye elimu ikiwemo michango ya chakula ili kuwezesha watoto wao kupata mlo wa mchana ili waweze kufanya vizuri katika masomo.
“Wananchi Hai tukishikamana tutaweza, lakini pia tushiriki maendeleo yetu kwa kuchangia licha ya kauli kuwa ‘elimu ni bure’, ila vipo vitu vya kuchangia ikiwemo chakula, hivyo niwasihi tuzingatie hili, katika kuhakikisha tunainua elimu yetu na kuyafikia maendeleo ya kweli.”
Diwani huyo anasema miongoni mwa wanasiasa anaovutiwa nao ni Halima Mdee na Ester Bulaya, ambao wanajiamini na hufanya mambo makubwa bila woga na wanawaelewa.