“NILIKUWA naona aibu sana kuja shuleni wakati wa hedhi, kilichonipa woga zaidi ni wenzangu watanionaje, Je nikiwa shuleni wakati wa kubadilisha kitambaa nitajifi cha wapi ili wenzangu wasinione?, Je nikichafuka wavulana si watajua nimepata hedhi.
“Bila shaka wanafunzi wataniona mkubwa sana, ni maswali yaliyonitesa kipindi nikiwa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Bukoba lakini kwa sasa sina wasiwasi kwani kuna sehemu ya kubadilishia vitambaa na mgao wa pedi kila mwezi,” anasema Rahima Faraja mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Bukoba.
Sekondari ya Bukoba ni moja ya shule kongwe nchini yenye mchanganyiko wa wasichana na wavulana inayojivunia maendeleo makubwa ya kutoa elimu kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, ikipiga hatua muhimu ya kupunguza utoro wa wanafunzi wa kike kila mwezi. Katika shule hiyo kumejengwa chumba maalumu cha kubadilishia vitambaa (taulo) vya hedhi pamoja na kutoa vitambaa vya hedhi kwa kila msichana kila mwezi.
Jambo hilo linaenda sambamba na utoaji wa elimu ya hedhi salama, uhamasishaji wa lishe bora pamoja na kuthaminiana na jinsi ya kumpatia huduma ya haraka mwanafunzi wa kike ambaye ameingia ghafla katika hedhi. Huduma hiyo hutolewa na wanafunzi wa kiume na wa kike katika hali isiyo na udhalilishaji tena.
Rahima anasema kila mwezi wakati akiwa kidato cha kwanza ilibidi atoe kikwazo kwa wazazi wake ili asiende shuleni wakati akiwa katika siku za hedhi kwani akujua atabadilisha vipi kitambaa na wanafunzi wakimgundua yuko katika hedhi atapata aibu kiasi gani.
Anasema kwa sasa hali ni tofauti, wanafunzi wa kike wote na wa kiume ujumuishwa pamoja na kupewa elimu ya hedhi, chumba maalumu cha wasichana kubadilishia vitambaa kipo na vitambaa ugaiwa kila mwezi lakini pia walimu wamekuwa mstari wa mbele kuwafundisha wanafunzi wa kiume kuwasaidia wasichana wanapokuwa katika hali hiyo.
Uwepo wa miundombinu hiyo umesaidia kupunguza utoro shuleni na hakuna msichana anayekosa shuleni kwa kukosa kitambaa cha kujisitiri au kukosa huduma hata akiingia kwa dharura kwani huduma inapatikana muda wote na kila mwanafunzi anapaswa kuwa huru.
Mwandishi wa makala haya alikutana na timu ya wanafunzi ambao huzunguka kutoa elimu kwa wanafunzi wenzao juu ya umuhimu wa msichana kupata hedhi na huwafundisha wasichana wa shule nyingine kuwa msichana kupata hedhi ni haki yake hivyo wasichana waache kujisikia dhaifu.
Naye mwanafunzi wa kidato cha nne wa shule hiyo, Florida Dezdery, anasema sasa kuingia katika hedhi si siri tena kama ilivyokuwa mwanzoni bali ni jambo la kawaida kwani amekuwa wazi kuwaambia hata wanafunzi wenzake juu ya kujisitiri kujiweka wazi na kujitunza pindi wanapokuwa katika hedhi.
Florida anasema amekuwa jasiri hata kuwaeleza wadogo zake na mabinti wengine mtaani namna bora ya kutengeneza vitambaa vizuri, namna ya kuvaa taulo za kike, namna ya kubadilisha wawapo katika shule zao hata kama zitakuwa hazina vyumba vya madarasa.
Mapendekezo yake kwa serikali ni kuhakikisha elimu ya hedhi salama inatolewa katika shule za msingi angalau kuanzia darasa la sita kwani baadhi ya wanafunzi wa kike wanapata hedhi kabla ya kumaliza darasa la saba pamoja na kuwawekea miundombinu bora ya kubadilisha vitambaa ili kuepusha uchafuzi na uzagaaji wa vitambaa hivyo.
Mwanafunzi mwngine, Angela Mugisha, anasema wakati yuko kidato cha kwanza alishuhudia vitambaa vikizagaa na kupeperushwa na upepo katika mazingira ya shule huku vikiwa vichafu, wasichana tuliona aibu na huu ni uchafuzi wa mazingira. Anasema kwa sasa hiyo hali haipo tena baada ya kuwepo sehemu maalumu ya kutupa vitambaa vilivyotumika.
Msimamizi na mtoa elimu ya hedhi katika Shule ya Sekondari Bukoba, Maria Shemkondo, anasema anafurahishwa na mahudhurio ya wanafunzi wa kike tangu kuboreshwa kwa mazingira ya shule hiyo kwani kipindi cha miaka ya nyuma mahudhurio yalikuwa yanapungua kila mwezi na wasichana hawakuweka wazi kilichokuwa kinawasibu zaidi ya kuomba ruhusa ya kuumwa bila kusema wanaumwa nini.
Anasema anaishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu hasa kwa watoto wa kike na kuendelea kuonesha kwamba watoto wote ni sawa kwani anashuhudia shule nyingi za manispaa ya Bukoba kukiwa na maendeleo na miundombinu kwa watoto wa kike juu ya ubadilishaji wa vitambaa vyao vya hedhi katika mazingira safi.
“Najisikia faraja kuona kwa sasa hakuna mwanafunzi anayekosa shule kwa sababu ya kukosa huduma shuleni hii ni tofauti na siku za nyuma kwa sasa kila mwezi tunapokea fedha za kununua vitambaa vya wasichana hivyo muda wowote wakijisikia wanachukua na wanatumia, kama mabinti wengi watashindwa kusoma kipindi hiki basi hawana wa kumlaumu kwa sababu kila kitu kiko sawa,” anasema Shemkondo.
Ombi la Shemkondo ni kwa taasisi zinazolenga kuboresha huduma ya hedhi salama kufikia shule zote za msingi na sekondari ambazo hazijafikiwa hasa za vijijini ili kujenga usawa na kuwafanya wasichana wajisikie kuwa wako sehemu salama na hedhi ni haki yao. Mkuu wa Shule ya Sekondari Bukoba, Raymond Mtakyawa, anasema shule hiyo hutenga asilimia 10 kila mwezi kutokana na fedha za elimu bila malipo kwa ajili ya kuwahudumia wanafunzi wa kike 497 na kueleza kuwa hawana upungufu wa vitambaa vya kike kwa miaka mitano mfululizo.
Mtakyawa anasema yeye akiwa mwalimu wa kiume, amekuwa wa kwanza kuwaongoza hata wavulana kutengeneza vitambaa vinavyoweza kumuhifadhi mwanamke kila mwezi jambo ambalo limewaweka pamoja kimasomo wanafunzi wa kike na kiume.
Anasema kwa sasa anafurahia kuona kuna kikundi jasiri cha Fema kilichoimarika ambacho kipo mstari wa mbele kuungana na shule nyingine za sekondari katika Manispaa ya Bukoba kwa ajili ya kuzungumzia kwa uwazi masuala ya hedhi salama.
“Hakuna utoro, miaka ya nyuma tulipata utoro sana wa wasichana, ulikuwa ukiwahoji baadhi ya wasichana walikuwa wakisema ukionekana unapata hedhi basi wenzako wanakuona umekuwa sana, wengi walipata aibu mpaka tulivyoanza kuongea hadharani, kugawa vitambaa hadharani na kutoa elimu pamoja na kuweka miundombinu ya kubadilishia hedhi sasa hakuna utoro hii ni habari njema sana kuona serikali inajali watoto wetu,”anasema Mtakyawa.
Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Manspaa ya Bukoba, Emmanuel Ebenezer anasema shule 34 za manispaa hiyo hupata taulo za kike (vitambaa vya kujisitiri) na kati ya shule hizo kwa sasa shule 32 za sekondari zote zina miundombinu ya kubadilishia taulo za kike na shule mbili ambazo hazina zinaendelea kuwekewa miundombinu hiyo mwaka huu.
Anasema mwaka 2018/2019 shule za sekondari zilipokea kiasi cha Sh bilioni 1.6 kwa ajili ya fedha ya elimu bila malipo kwa wanafunzi wa shule za sekondari na mwaka 2019/2020 manispaa ilipokea Sh bilioni 1.7 na fedha ambazo hutolewa kila mwezi asilimia 10 ya fedha hizo hutengwa kwa ajili ya kunua taulo za kike na dawa kwa ajili ya wanafunzi shuleni.
Anasema kwa sasa hakuna taarifa za utoro shuleni huku akisisitiza kuwa Manispaa ya Bukoba kupitia Idara ya Elimu inaendelea kuboresha miundombinu na kuhakikisha ufaulu wa wanafunzi wa kike unaongezeka.
Anakiri kuwa kwa sasa hakuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaoshindwa kufika kila mwezi shuleni isipokuwa kama kuna mwanafunzi wa kike anashindwa kufika shuleni ni changamoto nyingine na si suala ya hedhi.
“Nakiri kuwa siku za Nyuma kulikuwa na changamoto lakini kwa miaka hii ya uongozi wa serikali ya awamu ya tano miundombinu ya shule zetu imeboreshwa sana, wasichana wamepewa nafasi kubwa ya kusoma na kuishi katika miundombinu bora, ukweli ni kwamba asilimia 78 hadi 85 ya wanafunzi wa kike wanaochaguliwa kujiunga na sekondari, wanafika kidato cha nne,” anasema Ebenezer.
Ebenezer anasema huenda miaka ya nyuma ndoto za wengi zilipotea kutokana na kutokuwepo masuala ya hedhi salama shuleni. Mwaka 2018 utafiti uliofanywa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) unaonesha kuwa wasichana hukosa vipindi 400 kati ya 1,552 kila mwaka kutokana na ukosefu wa taulo za kike na mazingira bora ya kubadilisha taulo zao jambo ambalo husababisha kubaki nyumbani katika siku zao za hedhi.