Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hawara ateketeza nyumba, mtoto afia ndani

IMG 4398.jpeg Hawara ateketeza nyumba, mtoto afia ndani

Sat, 24 Jun 2023 Chanzo: Mwananchi

Mtoto Ashura Makelebe (4) amefariki dunia kwa kuteketea ndani ya nyumba kwa kile kinachodaiwa kuwa ni mtu anayedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mama yake kuamua kutekeza nyumba alimokuwa amelala.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Juni 23, 2023 na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Gideon Msuya, tukio hilo limetokea kwenye kisiwa cha uvuvi cha Kanyala Wilaya ya Sengerema.

Akifafanua, Kaimu Kamanda Msuya amesema mtuhumiwa Magesa Mukama ambaye tayari anashikiliwa na polisi kwa mahojiano aliamua kuteketeza nyumba hiyo baada ya kumkosa mama mzazi wa mtoto huyo alipoenda nyumbani kwake usiku wa kuamkia leo Juni 23, 2023.

Amesema mtuhumiwa alifikia uamuzi huo kutokana na wivu wa mapenzi baada ya kumkosa nyumbani mpenzi wake, Acyprian Charles (24) ambaye ndiye mama mzazi wa mtoto Ashura .

"Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa ambaye anashikiliwa kwa mahojiano zaidi alichukua uamuzi huo kutokana na wivu wa kimapenzi akihisi mpenzi wake ameenda kwa mwanaume mwingine,’’ amesema Kaimu Kamanda Msuya

Amesema pamoja na nyumba (kibanda) alimolala mtoto Ashura, moto huo ulisambaa na kuteketeza vibanda vingine 15 vya wavuvi vilivyokuwa jirani.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kanyala, Gacha Paul amewaomba wazazi kuwa makini kuhusu ulinzi na usalama wa watoto wao kwa kutowaacha wenyewe nyumbani wanapotoka nyakati za usiku.

‘’Baada ya kumhoji mama wa marehemu, amekiri kumwacha mtoto ndani ya nyumba akiwa amelala bila uangalizi wa mtu mwingine; hali iliyosababisha kifo chake kwa kuteketea ndani baada ya kibanda chao kushika moto. Siyo vema kumrushia lawama, lakini ni dhahiri kitendo cha kumwacha mtoto ndani ya nyumba mwenyewe usiku kimechangia janga hili,’’ amesema Gacha

Rafael Bituro, mmoja wa majirani amesema jitihada za kumwokoa mtoto Ashura hazikufanikiwa baada ya kuvunja mlango na kumkuta akiwa tayari amefariki kwa kuteketea kwa moto.

Chanzo: Mwananchi