Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Hausigeli’ watumikishwa kwa 20,000/- kwa mwezi

2ca881403d93c220d37c49e296e1a86f ‘Hausigeli’ watumikishwa kwa 20,000/- kwa mwezi

Mon, 15 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZAZI wa kike wakazi wa Bonde la Ziwa Rukwa katika Wilaya ya Sumbawanga, wanadaiwa kuwatumia mabinti wao kibiashara katika Mji wa Sumbawanga kwa malipo ya Sh 600 kwa siku.

Mkuu wa Dawati la Polisi la Jinsia,Wanawake na Watoto Mkoa wa Rukwa, Faustina Mwakapanga, aliyasema hayo katika kikao kilichojadili na kuweka mikakati kupambana na tatizo la mimba na ndoa utotoni.

Mwakapanga alisema wengi wa wasichana hao, wanatoka vijiji vya Bonde la Ziwa Rukwa wilaya ya Sumbawanga na kupelekwa mjini Sumbawanga.

Kikao hicho mjini Sumbawanga mwishoni mwa wiki kiliandaliwa na kuratibiwa na shirika lisilo la kiserikali la Peace Relief Organization (PRO) kwa ufadhili wa asasi ya kiraia ya Foundation for Civil Society (FCS).

Mwakapanga alisema watoto hao wa kike wenye umri kati ya miaka 14 na 16, wanafanya kazi za ndani kwa ujira wa Sh 20,000 kwa mwezi ikiwa sawa na malipo ya Sh 600 kwa siku na hawana mikataba ya kazi.

"Ukatili huu umejitokeza mkoani Rukwa, ni mfumo wa unyonyaji dhidi ya watoto hao kwani kilicho kibaya zaidi ni kwamba wazazi wa kike wa watoto hawa wanaingia makubaliano na "waajiri" wa watoto hao kwamba kiasi hicho cha shilingi 20,000 wawapatie wao (wazazi) kila mwezi...hivyo kwa maneno mengine watoto hao wanafanyishwa kazi bila malipo kwani wazazi wao wanazichukua zote" alisema.

Mwakapanga alisema, wengi wanaowatumikisha kazi za ndani watoto hao ni watumishi wa umma na wafanyabishara . Alisema watu hao wanakiuka Kifungu 155 (1)(2) cha Sheria ya Ndoa Sura 166.

Alisema, licha ya kutumikishwa bila mikataba, watoto hao wanafanyishwa kazi kwa zaidi ya saa 18 kila siku.

Wakichangia, baadhi ya washiriki walikiri kuwepo kwa visa hivyo vya ukatili dhidi ya watoto hao.

"Sio siri watoto hawa wanafanya kazi zote za nyumbani ikiwemo kufua nguo hadi za ndani za waajiri wao, watoto pia hupika na kazi zinginezo bila kuwa na muda wa kutosha wa kupumzika...huamka saa 11 alfajiri na hulala saa sita usiku "alisema mmoja wa washiriki, Yela Mwampamba.

Walisema watoto hao wamenyimwa haki ya elimu na kwamba wazazi wao wamewageuza kuwa chanzo cha kujiingizia kipato cha Sh 20,000 kila mwezi.

Chanzo: habarileo.co.tz